October 6, 2024

UDSM yawafungulia fursa ya ujasiriamali wahitimu elimu ya juu Tanzania

Ni kupatiwa mafunzo ya kuwawezesha kuanisha fursa zinazowazunguka ili wajiajiri.

  • Ni kupatiwa mafunzo ya kuwawezesha kuanisha fursa zinazowazunguka ili wajiajiri.
  • Watakutana na kujifunza kutoka kwa wajasiriamali wazoefu kutoka kwenye sekta mbalimbali.
  • Vijana wenye mawazo mazuri ya ujasiriamali wataunganishwa na watoa huduma za kifedha, teknolojia na uatamizi.

Dar es Salaam. Kama wewe ni mhitimu wa elimu ya juu Tanzania na una mpango wa kujiajiri katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali basi mlango umefunguliwa wa kupata uelewa, taarifa, maarifa, ujuzi na uwezo wa kuainisha fursa zinazokuzunguka na kuweza kuzitumia fursa hizo kuanzisha ajira na kuboresha maisha yako na jamii.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeandaa mafunzo ya ujasiriamali yatakayotolewa kwa wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu katika mikoa kumi ya Tanzania kuanzia Agosti hadi Oktoba mwaka 2019.

Taarifa iliyotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa  William Anangisye inaeleza kuwa mafunzo haya yanawalenga vijana wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu wenye nia ya kujenga uwezo na tabia ya kuona matatizo na changamoto kama fursa zitokanazo na taaluma zao.  

Katika mafunzo hayo yatakayotolewa katika makundi ya watu wasiozidi 50 kwa darasa kwa muda wa siku tatu mfululizo, washiriki watajifunza mbinu mbalimbali za kuanzisha na kuendeleza biashara. 


Zinazohusiana:


Pia watakutana na kujifunza kutoka kwa wajasiriamali wazoefu kutoka kwenye sekta mbalimbali kama vile, kilimo, ufugaji, madini, viwanda na huduma na kuwezeshwa kutengeneza mipango ya biashara ambayo itawasaidia kutafuta mitaji.  

“Kuwaunganisha vijana wenye mawazo mazuri ya ujasiriamali na watoa huduma za kifedha, teknolojia na uatamizi,” inaeleza taarifa hiyo. 

Mafunzo hayo yanatolewa bure ambapo mshiriki anatakiwa kuhudhuria mafunzo katika mkoa anaotoka au mikoa ya jirani, kwa mujibu wa UDSM mikoa iliyochaguliwa ni Katavi, Iringa, Mbeya, Dodoma, Mwanza na Arusha. 

Mikoa mingine ni Lindi, Dar es Salaam, Unguja Kaskazini na Unguja Kusini iliyopo visiwani Zanzibar. 

Huenda mafunzo hayo yakawasaidia vijana kuondokan ana tatizo la ajira na kuanzisha miradi itakayowatoa kimaisha badala ya kusubiri kuajiriwa.