November 24, 2024

Majaliwa aweka wazi ndoto aliyonayo kwa wasichana wa Ruangwa

Anataka kuona wanasoma hadi chuo kikuu ili warudi katika wilaya yao kuleta Maendeleo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Liuguru wilayani Ruangwa, Julai 29, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Anataka kuona wanasoma hadi chuo kikuu ili warudi katika wilaya yao kuleta Maendeleo.
  • Ameanza mkakati wa kuwajengea mabweni ili kuwakinga dhidi ya mimba za utotoni.
  • Pia shule mbili za sekondari za Mnacho na Liuguru zitabadilishwa ili zitumiwe na  wasichana tu. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema amekuwa na ndoto ya muda mrefu ya kuona shule ya Sekondari Liuguru iliyopo Wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi inabadilishwa na kuwa shule ya bweni kwa ajili ya wasichana ili kuwakinga dhidi ya changamoto mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni. 

Alikuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Liuguru wilayani Ruangwa jana jioni (Julai 29, 2019) mara baada ya kukagua shule hiyo, amesema azma hiyo ikifanikiwa itasaidia kutengeneza wanawake wengi wasomi na wachapa kazi. 

“Ndoto yangu ni kuona shule hii inakuwa ya wasichana peke yao. Na tukifanikiwa, tutatengeneza akinamama wasomi, wanaojitambua, wenye maadili mema na wachapakazi,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa amechagua shule za Mnacho na Liuguru ziwe ni za bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike kama njia ya kuwaongezea fursa za masomo katika wilaya hiyo.

“Leo nimekuja kuwaeleza ndoto yangu. Tunahitaji kuona kila mtoto anayeenda shule, anakuwa na uhakika wa kumaliza masomo yake ya elimu ya juu. Wilaya hii tuna shida ya idadi kubwa ya mimba kwa watoto wa kike, na mimi hili jambo linanikera sana,” amesema Majaliwa na kubainisha kuwa,

“Njia pekee ya kuondokana na tatizo hili ni kufanya shule hizi ziwe za bweni ili wakae hapa shuleni, wafundishwe bila kupoteza muda wa kwenda nyumbani au kukutana na vikwazo wawapo njiani kuja shule au kurejea nyumbani.”


Zinazohusiana: 


Amesema mabweni hayo yakikamilika wanafunzi wa kiume wanaosoma kwenye shule hizo mbili watahamishiwa katika shule zingine za jirani, ili wanafunzi wa kike wabaki peke yao. 

Akiwasilisha taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mwalimu Mkuu wa shule ya Liuguru, Samuel Diwani amesema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 ina walimu 11 ambapo watatu kati yao wanafundisha masomo ya sayansi na wanane waliobakia wanafundisha masomo ya lugha na sanaa.

Shule hiyo yenye wanafunzi 109 inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa nyumba tisa za walimu, ukosefu wa maabara mbili na iliyopo moja haijakamilika kwa asilimia 100.

“Nyingine ni ukosefu wa mabweni, maabara ya kompyuta, mfumo wa umemejua, maktaba, jengo la utawala na stoo,” amesema Mwalimu Diwani.