October 7, 2024

Magufuli aagiza mradi wa umeme wa Rufiji kukingwa na bima ya Serikali

Aziambia taasisi zinazohusika na mradi huo “ole wenu bima hiyo asaini mtu mwingine”.

  • Aziambia taasisi zinazohusika na mradi huo “ole wenu bima hiyo asaini mtu mwingine”.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameagiza mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mradi wa ufuaji umeme kwa maporomoko ya maji wa Rufiji kuhakikisha kuwa unakingwa na bima ya Serikali.

Rais aliyekuwa anahutubia katika uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo leo (Julai 26, 2019) amesema kumekuwa na mabishano baina ya Shirika la Bima la Taifa (NIC), Tanesco, wizara na wakandarasi kuhusu huduma za bima.

Hata hivyo, Rais hakueleza kwa kina mvutano huo wa bima baina ya taasisi hizo.

“Bima ya mradi huu asilimia 100 lazima itolewe na Serikali. Kwa hiyo Waziri (Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani) hili ulizingatie, wizara ya fedha mlizingatie, Tanesco mlizingatie…ole wenu mkatafute, akasaini bima na mtu mwingine,” amesema Rais Magufuli na kuongeza;

“Huu ni mradi wa Serikali na bima na guarantee (dhamana) lazima vitolewe na Serikali.”


Soma zaidi: 


Kwa mujibu wa Dk Kalemani hadi sasa Serikali imeshatoa asilimia 15 ya fedha zote za mradi huo sawa na Sh1.007 trilioni ya Sh6.5 trilioni.

Dk Kalemani amesema utekelezaji wa mradi huo unaendelea vema na iwapo kasi hiyo itaenda hivyo hivyo siku zijazo hapana shaka utakamilika ndani ya muda miezi 42 iliyopangwa ifikapo Juni 13, 2022.

Mradi huo wa kuzalisha umeme wa Megawati 2,115, unajengwa na kampuni za Misri ambazo ni El Sewedy and Arab Contractors ambazo zilishaanza hatua za awali za ujenzi miezi sita iliyopita.