October 7, 2024

Majaliwa awataka Ruvuma kuondoa vikwazo vya kiuwekezaji

Majaliwa amesema mkoa huo una fursa lukuki kama mikoa mingine ambazo zikiendelezwa, zitaleta tija na kusaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.

  • Amesema mkoa huo una fursa lukuki kama mikoa mingine ambazo zikiendelezwa, zitaleta tija na kusaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kuendelea kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo na kuondoa vikwazo vyote ili kuvutia wawekezaji zaidi.

Majaliwa aliyekuwa akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji mkoani Ruvuma linaloendelea kwenye uwanja wa Majimaji, Manispaa ya Songea leo (Julai 25, 2019) amesema mkoa huo una fursa lukuki kama mikoa mingine ambazo zikiendelezwa, zitaleta tija na kusaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.

“Nitoe rai kwa mkoa uendelee kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo sambamba na kuondoa vikwazo vyovyote vya uwekezaji na biashara ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje,” amesema Majaliwa katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia mkaa wa mawe, uliyotengenezwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na wajasiriamali wa kikundi cha Mbalawala Women Group, wakati akikagua mabanda kwenye maonesho ya viwanda na kongamano la uwekezaji mkoani Ruvuma, Julai 25.2019. Tokea kulia ni Meneja wa Fedha wa kikundi hicho, Esta Silas na Msimamizi wa Mradi, Hajra Yakub. Picha |Ofisi ya Waziri Mkuu).

Amesema katika ustawi wa uchumi, nchi nyingi ulimwenguni zikiwemo Marekani, China, Japan, Korea ya Kusini na Ujerumani zimeweza kukuza uchumi wao kupitia ujenzi wa viwanda na zimefanikiwa kupunguza umaskini katika jamii zao.

“Tunapaswa kuiga kutoka wa wenzetu. Ndiyo maana Tanzania pia tunahamasisha ujenzi wa viwanda kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mikoa ili tulete mageuzi ya kiuchumi yatakayowezesha upatikanaji wa ajira na hatimaye kuondoa umaskini,” amesema kiongozi huyo katika kongamano hilo lenye kaulimbiu “Ruvuma itavuma kwa uchumi wa viwanda, wekeza sasa.”


Soma zaidi:


Kongamano hilo limelenga kutangaza fursa za uwekezaji na biashara zilizopo mkoani humo likiwa na lengo la kutekeleza azma ya Serikali ya Rais John Magufuli ya kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo 2025.

Amesema mchango wa sekta ya viwanda kiuchumi na kijamii nchini ni pamoja na kuongeza pato la Taifa na kupandisha hali ya maisha ya wananchi; kusaidia nchi isiyumbe kiuchumi ikizingatiwa kuwa viwanda vingi havitegemei hali ya hewa kama kilimo; kuboresha urari wa biashara (balance of trade) kwa sababu tija yake ni kubwa na hasa bidhaa nyingi zikiuzwa nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Mwakilishi wa Balozi wa China, Xian Ding ameahidi kuwapeleka wawekezaji kutoka China “kwa sababu tunataka waje kuleta teknolojia mpya, wafanye kazi pamoja na Watanzania na wawafundishe teknolojia hizo mpya. Tunataka hapa Ruvuma iwe model (mfano) kwa mikoa mingine.”

Kwa muda mrefu wafanyabiashara nchini wamekuwa wakilalamikia kutokuwapo mazingira rafiki ya biashara kutokana na kuwepo vikwazo kutoka kwa miongoni mwa viongozi na taasisi za umma huku Serikali ikiahidi kuondoa vikwanzo hizo.