Magufuli amrejesha bosi TPDC madarakani miaka mitatu baada ya kusimamishwa
Kigogo huyo na wenzie wanne wa TPDC walisimamishwa na Bodi ya Wakurugenzi kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi.
Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Dk James Mataragio. Picha|Mtandao.
- Rais amesema Dk James Mataragio arudishwe mara moja katika nafasi yake hiyo.
- Kigogo huyo na wenzie wanne wa TPDC walisimamishwa na Bodi ya Wakurugenzi kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi.
Dar es Salaam. Miaka mitatu baada ya kusimamishwa kazi, Dk James Mataragio, Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), ni moja ya watu wenye furaha zaidi nchini kwa sasa.
Furaha hiyo inakuja baada ya Rais John Magufuli kuiagiza Wizara ya Nishati kumrudisha kigogo huyo mara moja katika nafasi yake aliyoondolewa Agosti 2016 kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi.
Dk Mataragio na vigogo wengine wanne wa juu wa TPDC walisimamishwa na Bodi ya Wakurugenzi mwaka 2016 kutokana shutuma za matumizi mabaya ya ofisi ikiwemo kufanya manunuzi kinyume na sheria na kujipatia manufaa yasiyo ya halali ya dola za Marekani 3,238,986.50 sawa na takribani Sh7.4 bilioni.
Vigogo wengine walikuwa Meneja Utafutaji, George Semi; Mkuu wa Manunuzi na Utawala, Wellington Hudson; Mkurugenzi wa Idara ya Fedha, Kelvin Komba; na Mkurugenzi wa Mipango Mkakati, Edwin Riwa.
Machi mwaka jana vigogo hao watano walipandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkaazi Kisutu kwa tuhuma hizo ambazo walizikana.
Soma zaidi: TPDC yafungua fursa ya uwekezaji vituo vya gesi asilia Tanzania
Kwa kipindi chote hicho, Dk Mataragio huenda hakuwahi kufikiria katika utawala wa Rais Magufuli angeweza tena kurejea katika madaraka yake ya awali hasa kutokana na vita kali dhidi ya ufisadi na uzembe kazini.
Hata hivyo, jana (Julai 22, 2019), Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa alitoa taarifa kuwa Dk Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati kumrudisha Dk Mataragio katika nafasi yake hiyo.
“Katika agizo hilo, Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Nishati kumrejesha Dk Mataragio katika nafasi yake ya Mkurugenzi Mkuu wa TPDC ili aendelee na majukumu yake,” imesema taarifa hiyo ya Ikulu.
Hata hivyo, hadi sasa haijafahamika bayana hatma ya vigogo wengine wanne waliosimamishwa pamoja na Dk Mataragio miaka mitatu iliyopita.
Kwa kipindi chote hicho wakati Dk Mataragio akiwa amesimamishwa kazi, TPDC ilikuwa ikiongozwa na Kapuulya Musomba aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo.