October 6, 2024

Mauzo soko la hisa Dar yapaa

Yameongezeka kwa asilimia 99.9 hadi kufikia Sh948.4 milioni kutoka Sh506,500 iliyorekodiwa mwishoni mwa wiki inayoishia Julai 19, 2019.

  • Yameongezeka kwa asilimia 99.9 hadi kufikia Sh948.4 milioni kutoka Sh506,500 iliyorekodiwa mwishoni mwa wiki inayoishia Julai 19, 2019.
  • CRDB yaongozwa kwa mauzo yanayofikia Sh467.9 milioni.

Dar es Salaam. Mauzo katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) yameongezeka kwa asilimia 99.9 hadi kufikia Sh948.4 milioni kutoka Sh506,500 iliyorekodiwa mwishoni mwa wiki inayoishia Julai 19 mwaka huu huku benki ya CRDB PLC ikiongoza kwa kuuza hisa nyingi. 

Ripoti ya siku ya DSE iliyotolewa leo (Julai 22, 2019) inaonyesha kuwa kupanda kwa mauzo hayo kumetokana na ongezeko la idadi ya hisa zilizouzwa leo sokoni. 

Idadi ya hisa zilizouzwa leo sokoni zilikuwa 4,596,080 ambapo zimeongezeka kutoka hisa 281 zilizouzwa Julai 19 wakati soko linafungwa. 

Katika mauzo hayo ya leo, benki ya CRDB ndiyo imekuwa kinara wa kuuza hisa nyingi ikiwa ni asilimia 98.4 ya hisa zote na kuifanya iongoze kwa mauzo kwa kuweka kibindoni Sh467.9 milioni ya mauzo yote. 

Kampuni nyingine ambazo zilikuwa na mauzo ya juu ni pamoja na kampuni ya bia Tanzania (TBL) iliyouza hisa zenye thamani ya Sh283.2 milioni, kampuni ya sigara ya TCC (Sh134.8 milioni) na TPCC (Sh58.6 milioni). 

Kutokana na mauzo hayo ya leo, mtaji wa soko hilo umeongezeka hadi kufikia Sh19.2 trilioni kutoka Sh18.9 trilioni yaliyorekodiwa ijumaa iliyopita.


Zinazohusiana: 


Wakati mauzo ya DSE yakiongezeka, kampuni ya Acacia imefanya vizuri sokoni leo baada ya thamani ya hisa zake kuongezeka na kuwafanya wawekezaji wa kampuni hiyo kulala na tabasamu kwa kupata Sh350 kwa kila hisa moja. 

Hisa moja ya Acacia imeuzwa kwa Sh6,350 kutoka Sh6,000 iliyorekodiwa ijumaa iliyopita lakini kampuni hiyo haikufanikiwa kuuza hata hisa moja leo sokoni. 

Kampuni nyingine ambazo thamani ya hisa zake imepanda ni pamoja na Kenya Airways ambayo imepanda kwa asilimia 4.76, TPCC (asiulimia 3), benki ya KCB (asilimia 2.33) na kampuni ya bia ya Afrika Mashariki-EABL (asilimia 0.23). 

Hata hivyo, wawekezaji wa kampuni ya USL watalala na maumivu baada ya thamani ya hisa za kampuni hiyo kushuka kwa asilimia 50 akifuatiwa na kampuni ya JHL ambayo hisa zake zimeshuka kwa asilimia 0.61.