October 6, 2024

Karatu waanza kujenga vituo vya kuwalinda watalii

Vituo hivyo maalum vitawaondolewa usumbufu wa kukaguliwa mara kwa mara wakiwa barabarani.
Pia vitawaongezea usalama wakiwa katika shughuli za utalii.

  • Vituo hivyo maalum vitawaondolewa usumbufu wa kukaguliwa mara kwa mara wakiwa barabarani.
  • Pia vitawaongezea usalama wakiwa katika shughuli za utalii. 
  • TATO watoa gari kwa ajili ya dolia

Dar es Salaam. Halmashauri ya Wilaya ya Karatu imezindua ujenzi wa vituo vinne vya polisi vitakavyotumika kwa ajili ya ukaguzi wa watalii ili kuwahakikishia usalama na kuwapunguzia usumbufu wa kukaguliwa wakiwa katika shughuli za utalii nchini.  

Ujenzi huo umezinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana (Julai 22, 2019) katika eneo la Bashay katika Wilaya ya Karatu mkoani Arusha ikiwa ni hatua ya kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa amezindua kituo cha kutolea huduma za usalama kwa watalii wilayani Karatu ikiwa ni ishara ya kuwakilisha vituo vingine vitatu vinavyoendelea kujengwa mkoani Arusha katika maeneo ya Kikatiti (Arumeru), Makuyuni (Monduli) na Engikaret (Longido).

Pia amewashukuru viongozi wa Chama cha Waendesha shughuli za Utalii Tanzania (TATO) kwa kuchangia ujenzi wa vituo hivyo na kutoa gari jipya la polisi kwa ajili kituo hicho cha Karatu.

Gari hilo aina ya Toyota Landcruiser lililogharimu dola za Marekani 45,000 (takriban Sh103.5 milioni), limepewa namba za usajili za PT 4190.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizindua kituo cha huduma za utalii wilayani Karatu, katika Mkoa wa Arusha, Julai 21.2019. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema ujenzi wa vituo hivyo umetokana na malalamiko aliyopokea kutoka kwa watalii kuwa wakitoka uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) hadi kufika Karatu wanakuwa wamesimamishwa njiani zaidi ya mara 20.

 “Tulijiuliza hawa watalii wamekuja kutalii, wanataka kupumzika, sasa ni kwa nini wasumbuliwe kiasi hicho? Tuliamua kuanzisha vituo vya aina hii, ili watalii wafanyiwe ukaguzi kwenye check-points (vituo vya ukaguzi) maalum,” alisema.

 Ameliomba Jeshi la Polisi liwapange barabarani askari ambao ni weledi na wana uelewa wa masuala ya utalii na kutolea mfano wa wiki iliyopita ambapo alikuwa akitokea mjini kwenda Karatu na kukuta magari ya watalii zaidi ya 10 yamesimamishwa njiani.

 “Niliona baadhi yao wakiwa wamelala kwenye magari kwa uchovu, nilipowauliza wamekalishwa kwa muda gani, walisema ni kwa zaidi ya dakika 45. Nilipomuuliza askari aliyewasimamisha ni kwa nini anafanya hivyo, akanijibu kwamba dereva amemjibu vibaya. Hivi ni kwa nini watalii wateseke juani wakati mwenye makosa ni dereva?,” ameuliza Gambo. 


Zinazohusiana: 


Naye, Makamu Mwenyekiti wa TATO, Henry Kimaro aliishukuru Serikali kwa jitihada inazofanya za kupambana na ujangili na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.

 “Tumeona hivi karibuni watalii wengine kutoka Israel, China na sasa ndege yetu imeanza kwenda India kuwafuata huko huko,” amesema Kimaro.

 Amebainisha  kuwa wameanza na vituo hivyo vinne mkoani Arusha lakini tatizo hilo liko maeneo mengi nchini na wao hawawezi kufika nchi nzima kutoa huduma kama hiyo. 

 Amemuomba Waziri Mkuu awahimize wakuu wa wilaya ambao wilaya zao zinajihusisha na sekta ya utalii, waige mfano wa wilaya ya Karatu ili kuhakikisha usalama wa watalii wawapo nchini.

 Katika hatua, nyingine Waziri Mkuu, amewataka wakazi wa Bashay, watumie fursa ya ujenzi wa vizimba vya biashara vya kuuzia bidhaa za utalii zitakazowawezesha kupata kipato na kuboresha maisha yao.

“Tumieni fursa ya uwepo wa eneo hili. Halmashauri wakishajenga vizimba vya biashara, leteni bidhaa zenu kama vile picha za tingatinga, mapambo, vinyago na vyakula vya asili ili watalii wakija hapa wapate huduma kutoka kwenu,” amesema Majaliwa.

Amewataka wakazi hao wawalinde watalii ili waitangaze vema nchi ya Tanzania pindi wakirudi makwao kwa kuhakikisha wanakuwa salama wakati wote. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikata utepe kuzindua rasmi  kituo cha huduma za utalii wilayani Karatu, katika Mkoa wa Arusha, Julai 21.2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.