October 6, 2024

Nyaraka za ardhi sasa kutolewa ngazi ya mkoa

Serikali itaanza kusajili nyaraka za ardhi ndani ya mikoa badala ya utaratibu wa awali katika kanda maalum ili kurahisisha upatikanaji wa nyaraka hizo

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi akizungumza leo (Julai 19, 2019) Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa wataalamu wa sekta ya ardhi. Picha|Mtandao.


  • Serikali itaanza kusajili nyaraka za ardhi ndani ya mikoa badala ya utaratibu wa awali katika kanda maalum.
  • Utasaidia upatikanaji wa nyaraka hizo kwa wakati na kwa urahisi.
  • Kwa kila Watanzania 10 takriban sita hawana nyaraka kuonyesha wanamiliki ardhi au makazi.

Dar es Salaam. Huenda idadi ya Watanzania wenye nyaraka za umiliki ardhi ikaongezeka, baada ya Serikali kuanza mchakato wa kuhamisha ofisi za kusajili nyaraka za ardhi kutoka ngazi ya kanda hadi mikoani. 

Hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa nyaraka za ardhi ikiwemo hati za nyumba na makazi, ikizingatiwa kuwa bado Watanzania wengi  hawana nyaraka hizo. 

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa tathmini ya haki na usalama wa ardhi kwa ajili ya makazi (Tanzania Baseline Survey Report on Assessment of Land Rights And Tenure Security 2018) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa zaidi ya nusu ama asilimia 55 ya wananchi waliohojiwa hawana nyaraka muhimu kuthibitisha haki yao ya kutumia au kumiliki makazi au ardhi wanayoikalia. 

Hiyo ni sawa na kusema kwa kila Watanzania 10 basi takriban sita hawana nyaraka kuonyesha wanamiliki ardhi au makazi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi amesema Serikali itaanza kusajili nyaraka za ardhi ndani ya mikoa ya Tanzania badala ya utaratibu wa awali ambapo zoezi hilo lilikuwa linafanyika katika kanda maalum.

Amesema wamekusudia kuhamisha ofisi za kusajili nyaraka za ardhi ili kurahisisha upatikanaji wa nyaraka hizo kwa wakati na tayari Wakuu wa Mikoa wameridhia na kutoa majengo yatakayotumika kama ofisi za wizara za usajili katika mikoa yao.

“Serikali imeamua kuunda ofisi za ardhi ngazi ya mkoa  na sio kanda kama ilivyokuwa awali,” amesema Lukuvi leo (Julai 19, 2019) Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa wataalamu wa sekta ya ardhi. 

Amesema michoro yote ya ardhi sasa itapitishwa mkoani, taarifa za uthamini wa ardhi  ambazo zilikuwa zinapatikana makao makuu sasa atateuliwa mthamini mkuu kila mkoa.


Soma zaidi: Zaidi ya nusu ya Watanzania hawana nyaraka za umiliki wa ardhi


Amemtaka Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Doroth Mwanyika kuhakikisha anapanga safu ya wakuu wa idara watakaokwenda kufanya kazi katika ofisi za wilaya na ofisi za mipango miji na orodha hiyo ipite mikononi mwake kabla ya wahusika kupewa barua za uteuzi.

Katika  kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki, amepiga marufuku wakuu wa idara za ardhi kupokea tozo ambazo hazistahili pamoja na utumiaji wa madalali ndani ya ofisi za umma.

“Nimekuta baadhi ya halmashauri mtu anatozwa zaidi ya 500,000 ili apate kibali cha ujenzi huu ni unyonyaji. Nitakula sahani moja na kila mtu bado kuna madudu mengi sana kwa watumishi wa ardhi,” amesema.

Mkutano huo wa wataalam wa ardhi umelenga kutathmini wapi walipo na malengo ya sekta hiyo, sambamba na kuwajengea uwezo wataalam  hao namna bora ya ufanyaji  kazi na namna ya kutatua changamoto zilizopo.