October 6, 2024

Majaliwa awakalisha kiti moto watumishi wa umma Same

Ataka wawe na mipango kazi, asema Serikali inapima matokeo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongea na Viongozi na Watumishi wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, katika ukumbi wa Halmashauri Julai 19.2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Ataka wawe na mipango kazi, asema Serikali inapima matokeo.
  • Amewataka watumishi hao watambue falsafa ya kiongozi mkuu wa nchi ambayo inahimiza uchapakazi. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma nchini Tanzania wawe na mipango ya kazi ambayo itaweza kupimika na kutoa matokeo katika shughuli zao za kuwatumikia wananchi. 

Pia amewataka watambue mipaka yao na wajenge mahusiano baina yao na wengine kulingana na nafasi zao za kuteuliwa, kuajiriwa na kuchaguliwa. 

“Kila mtumishi anapaswa awe na mpango kazi katika sekta yake na ni lazima aende kupima matokeo. Awamu hii, tunataka kuona matokeo ya kazi zenu,” amesema Majaliwa leo (Julai 19, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Same, mkoa wa kilimanjaro. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu,  ametumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi hao kuwa baada ya mchujo wa watumishi hewa, waliobakia wanapaswa kufanya kazi kwa bidii. 

“Watumishi mmeletwa kwenye wilaya hii ili muwahudumie wananchi. Tulioajiriwa, kazi yetu kubwa ni kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wowote uwe ni wa kabila, itikadi au rangi.

“Fanyeni kazi kwa bidii, msimamo wa Serikali hii ni kwamba hatumvumilii mtumishi ambaye si mwajibikaji, ni mwizi, mzembe au anaomba rushwa. Serikali hii hatuna muda wa kujadili matatizo ya watumishi, tunamalizana hapo hapo,” amesema. 


Soma zaidi: 


Amesema watumishi hao wasimamie utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa sababu ndiyo chama tawala. 

Kuhusu tabia ya baadhi ya watumishi kukaa ofisini, Waziri Mkuu amekemea tabia hiyo na kuwataka watumishi wote nchini waache tabia ya kukaa ofisini na badala yake waende vijijini kuwasikiliza wananchi. 

Amewataka watumishi hao watambue falsafa ya kiongozi mkuu wa nchi ambayo inahimiza uchapakazi. 

“Kwa hiyo tunaposema Hapa Kazi Tu, maana yake chapa kazi na tuone matokeo. Tunasisitiza kazi na tunataka kazi unayoifanya, itoe matokeo,” amesisitiza.