October 7, 2024

Misri yafungua tena mapiramidi mawili ya zamani kuchochea utalii

Yanapatika takriban kilomita 40 Kusini mwa jiji la Cairo ambapo moja ni ile iliyoinama ya Pharao Snerefu na ya pili ipo Dahshur Necropolis mjini Giza.

Piramidi iliyoinama ya Pharao Snerefu. Picha|AP.


  • Yanapatika takriban kilomita 40 Kusini mwa jiji la Cairo
  • Piramidi moja ni ile iliyoinama ya Pharao Snerefu na ya pili ipo Dahshur Necropolis mjini Giza. 
  • Mapiramidi hayo yatachochea utalii, baada ya machafuko ya kisiasa mwaka 2011.

Nchi ya Misri imefungua mapiramidi mawili kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1965 baada ya kukamilisha mchakato wa kuyakarabati ili yatumike kwa ajili ya shughuli za utalii. 

Mapiramidi hayo yanapatika takriban kilomita 40 Kusini mwa jiji la Cairo ambapo uzinduzi wake ulihudhuriwa na viongozi wa Serikali na Wanadiplomasia wa kigeni. 

Waziri wa mambo ya Kale, Khaled al-Anani akizungumza katika ufunguzi huo amesema piramidi moja ni ile iliyoinama ya Pharao Snerefu na ya pili ni piramidi inayosemekana ni ya kwanza iliyopo Dahshur Necropolis mjini Giza. 

Piramidi hiyo iliyoinama yenye urefu wa mita 101 ni kielelezo cha mapiramidi ya kwanza yaliyojengwa nchini Misri ambapo lilijengwa na Pharaoh Snerefu aliyekuwa mwasisi wa kizazi cha nne cha ufalme wa Misri enzi za ufalme wa zamani miaka 2600 kabla ya Kristo.


Soma zaidi: Watumia miaka mitano kuchimba sanamu ya miaka 300 Misri


Wakati akiongea na Wanahabari jumamosi (Julai 13, 2019), Al-Anani alisema kuwa mapiramidi hayo kwa pamoja yameorodheswa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuwa ni majengo na makaburi ya kale kabisa ya Memphis. 

Amesema pia watalaam wa mambo ya kale wamegundua kuwepo kwa mkusanyiko wa mawe, udongo na malighafi za mbao kwenye piramidi la Dahshur Necropolis mjini Giza.

Vitu vingine ambavyo vimepatikana ni pamoja na vifaa vya kufunika kichwa na kukatia mawe, ambapo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mambo ya Kale, Mostafa Waziri amesema wataendelea na kazi ya kuchimba ili kubaini vitu vingine Agosti mwaka huu. 

Misri ina matumaini kuwa uvumbuzi huo utachochea ukuaji wa sekta ya utalii ambao kwa kiasi kikubwa unaendeshwa na rasilimali za mambo ya kale ambazo ziliharibiwa vibaya wakati wa machafuko ya kisiasa mwaka 2011.