Hii ndiyo mikoa 10 iliyoshika mkia matokeo ya kidato cha sita
Mikoa hiyo ni pamoja Dar es Salaam, Mbeya na Kaskazini Pemba ambao umeshika mkia kitaifa.
- Mkoa wa mwisho kitaifa ni Kaskazini Pemba.
- Mikoa mingine ni Dar es Salaam, Mbeya na Mjini Magharibi.
- Lindi, Mtwara, Geita waingia katika orodha ya mikoa 10 bora kitaifa.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya kidato cha sita, leo limetoa orodha ya mikoa 10 iliyofanya vibaya katika mtihani huo ikiongozwa na mkoa wa Kaskazini Pemba ambao umekuwa wa mwisho kitaifa.
Kwa mujibu wa mpangilio wa mikoa kwa ubora wa ufaulu katika mtihani wa kidato cha sita 2019 uliotolewa na Necta leo (Julai 12, 2019) unaonyesha kuwa mkoa wa Kaskazini Pemba umeshika mkia kati ya mikoa 29 iliyoshiriki mtihani huo.
Katika matokeo ya mwaka jana, mkoa huo ulishika nafasi ya 28 lakini mwaka huu umeporomoka hadi nafasi ya mwisho.
Mikoa mingine iliyofanya vibaya ni pamoja Kusini Pemba, Mjini Magharibi yote ya visiwani Zanzibar. Mjini Magharibi pia umetoa shule nne ambazo zimeingia katika orodha ya shule 10 zilizofanya vibaya kitaifa.
Mikoa ya Tanzania bara ambayo nayo imeingia kwenye orodha hiyo ni Katavi, Mara, Shinyanga, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Dar es Salaam.
Licha ya Dar es Salaam kuwa katika orodha hiyo, imetoa shule tatu ambazo zimeingia katika orodha ya shule 10 bora kitaifa mwaka huu.
Soma zaidi:
Wakati viongozi wa mikoa hiyo wakitafakari matokeo hayo, wenzao wa Lindi leo watalala na tabasamu baada ya mkoa huo kuongoza kitaifa katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde.
Lindi imekuwa ya kwanza kitaifa mwaka huu baada ya kupanda nafasi moja kutoka nafasi ya pili iliyoshika mwaka 2018 ambapo imeungana na mikoa mingine 9 kuunda orodha ya dhahabu ya mikoa bora kwa ufaulu Tanzania.
Mkoa wa Singida umeshika nafasi ya pili ukifuatiwa na Mtwara ambao umeporomoka kutoka nafasi ya kwanza iliyoshikilia mwaka jana. Mikoa mingine ni Geita, Manyara, Ruvuma, Arusha, Tabora, Kilimanjaro na Simiyu.
Orodha ya mikoa kulingana na ufaulu wake katika mtihani wa kidato cha sita. Picha|NECTA.