October 6, 2024

TANTRADE kuwaunganisha wajasiriamali na masoko ya kimataifa

Mamlaka hiyo ya biashara nchini imesema itaendelea kuwasaidia wafaidike na fursa mbalimbali ikiwemo masoko.

  • Mamlaka hiyo ya biashara nchini imesema itaendelea kuwasaidia wafaidike na fursa mbalimbali ikiwemo masoko. 
  • DHL Tanzania kuwapa jukwaa la kimataifa kutangaza biashara zao. 
  • Balozi Iddi aitaka kuongeza juhudi za kuwasaidia wajasiriamali kukuza biashara zao.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imesema itaendelea kuimarisha mitandao ya wadau na kampuni mbalimbali nchini ili kuhakikisha wajasiriamali wadogo nchini wanapatiwa fursa za kuuza bidhaa kwenye masoko ya kimataifa. 

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Zanzibar, Latifa Khamis amesema mamlaka hiyo itaendelea kutumia majukwaa na fursa mbalimbali za kibiashara kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali kutumia fursa zilizopo ili huduma na bidhaa zao zipate masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi.

Khamis alikuwa akizungumza wakati wa mkutano wa wafanyabiashara, wazalishaji na wanunuzi wa bidhaa za ngozi na shule katika Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere.

“TANTRADE imeandaa mkutano huu maalum kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo kuweza kupata fursa za masoko ya kuuzia bidhaa zao ambapo utaratibu huu utakuwa endelevu,” amesema Khamis.

Amesema mara baada ya kukamilika kwa maonyesho ya 43 ya DITF, TANTRADE imeandaa mkakati maalum wa kuwaunganisha wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara kupitia maonyesho ya bidhaa za wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo nchi nzima ambapo wataanzia katika mkoa wa Ruvuma na baadaye Zanzibar.


Zinazohusina: 


Mkutano huo uliofanyika jana (Julai 11, 2019) pia uliwakutanisha wafanyabiashara, wajasiriamali wadogo na taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo Benki ya NMB ambayo imekuwa na utaratibu wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali ili kuendeleza biashara zao. 

Meneja Mkazi wa Kampuni ya DHL Tanzania, Paul Makolosi ambaye alishiriki katika mkutano huo, amewataka wafanyabiashara wadogo kutangaza bidhaa zao katika kampuni hiyo kwa sababu ina mtandao mpana katika nchi nyingi za Ulaya na Amerika ambazo zimekuwa zikivutiwa na bidhaa zinazozalishwa katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.

DHL Tanzania inaendesha jukwaa la mtandaoni la  MarketPlace Africa ambalo linatoa fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali  kutangaza biashara zao. 

Makalozi amesema kampuni hiyo ina uzoefu wa miaka 30 ya kufanya biashara duniani, ambapo katika utendaji kazi wake imekuwa ikiwasaidia zaidi wajasiriamali wadogo waliopo Afrika, hivyo ujio wa taasisi hiyo hapa nchini ni fursa kwa wajasiriamali kukuza biashara zao kimataifa.

“Katika nchi za bara la Ulaya na Amerika, bidhaa za ngozi hususan viatu vimekuwa na soko kubwa sana, na kwa kuwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wa hapa Tanzania wamekuwa wakizalisha bidhaa hiyo, sisi DHL kupitia MarketPlace Africa tupo tayari kuwasaidia ili kupata masoko ya uhakika,” amesema Makolosi.Sehemu ya kuingilia katika Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere. Picha|Mtandao.

Mikakati hiyo ya TANTRADE huenda ikiwa ni mwanzo wa utekelezaji maagizo ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Iddi ambaye aliitaka mamlaka hiyo kuimarisha mitandao na mifumo ya biashara itakayowawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kuwa na uhakika wa masoko ya bidhaa zao.

Balozi Iddi alitoa maagizo hayo jana wakati akifunga maonyesho ya biashara ya Saba Saba ambayo hufanyika kila mwaka jijini Dar es Salaam ambapo mwaka huu kampuni 3,250 zilishiriki maonyesho hayo.