October 6, 2024

Ufaulu masomo manne washuka kidato cha sita

Masomo hayo ni General Studies, Historia, Bailojia na Accountancy ambayo ufaulu wake umeshuka kwa viwango tofauti.

  • Masomo hayo ni General Studies, Historia, Bailojia na Accountancy.
  • Ufaulu wake umeshuka kwa viwango tofauti ukilinganisha na mwaka 2018. 
  • Masomo ambayo ufaulu wake umepanda ni pamoja na Geografia, Kiswahili, English na Kemia. 

Dar es Salaam. Matokeo ya kidato cha sita mwaka 2019 yaliyotangazwa leo yanaonyesha kuwa ufaulu wa watahiniwa katika masomo manne, likiwemo la General Studies ambalo huchukuliwa poa na wanafunzi, umeshuka kwa viwango tofauti ukilinganisha na mwaka jana. 

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde ameyataja leo (11 Julai 2019) masomo ambayo ufaulu umeshuka ni pamoja na General Studies, Historia, Biolojia na Accountancy. 

Amesema ufaulu wa somo la General Studies umeshuka kutoka asilimia 94.45 mwaka 2018 hadi asilimia 92.14 mwaka huu ambapo somo la Historia, ufaulu wake umeshuka kutoka asilimia 99.05 hadi 96.91. 

Somo la Baiolojia ambalo ni miongoni mwa masomo ya sayansi ufaulu wake umeshuka kiduchu kutoka asimia 96.98 mwaka 2018 hadi asilimia 96.12 mwaka huu. 


Soma zaidi: 


Somo lingine ambalo ufaulu wake umeporomoka ni ‘Accountancy’ (Uhasibu) ambapo umeshuka kutoka asilimia 96.51 hadi asilimia 96.08 mwaka huu. 

Wakati masomo hayo manne ufaulu wake ukishuka, ufaulu wa masomo 14 yaliyobaki umepanda likiwemo somo la Advanced Mathematics ambalo limekuwa likiwatoa jasho wanafunzi wengi. 

Ufaulu wa somo hilo umepanda hadi asilimia 86.74 mwaka huu kutoka asilimia 83.74 iliyorekodiwa mwaka 2018. 

Masomo mengine ambayo ufaulu wake umepanda ni pamoja na Geografia, Kiswahili, English na Kemia.