November 24, 2024

Hizi ndizo shule 10 bora kidato cha sita mwaka 2019

Shule za Kisimiri na Feza hazijawi kutoka katika orodha ya kumi bora toka mwaka 2012.

  • Shule za Kisimiri na Feza hazijawahi kutoka katika orodha ya 10 bora toka mwaka 2012.
  • Shule za  Marian Girls na Marian Boys zang’ooka katika orodha hiyo.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita ya mwaka 2019 huku shule ya Sekondari ya Kisimiri ya mkoani Arusha ikiongoza matokeo hayo.

Akitangaza matokeo hayo leo (Julai 11, 2019) Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde amezitaja shule 10 zilizofanya vizuri zaidi katika matokeo hayo kuwa ni  Kisimiri (Arusha), Feza Boys (Dar es Salaam), Ahmes ( Pwani) Mwandet (Arusha), Tabora Boys(Tabora) na Kibaha (Pwani). 

Nyingine katika orodha hiyo ni Feza Girls (Dar es Salaam) ,St Mary’s Mazinde Juu (Tanga) , Canossa (Dar es Salaam) na  Kemebos ( Kagera.)

Katika orodha hiyo Dar es Salaam inaongoza kwa kuwa na shule tatu wakifuatiwa na Arusha na Pwani yenye shule mbili kila moja. 

Katika matokeo hayo shule za Kisimiri na Feza Boys zimeendelea kuwa vinara  katika katika 10 bora kitaifa kwa mwaka wa nane mfululizo toka mwaka 2012, licha ya kupata ushindani mkali wa shule zingine kongwe ikiwemo Kibaha ambayo imefanikiwa kuingia mara saba toka mwaka 2012.


Zinazohusiana: 


Pia matokeo ya mwaka huu yameshuhudia ingizo jipya la Shule ya Sekondari ya Mwandet kutoka mkoani Arusha katika iliyoshika nafasi ya nne kitaifa na kuziacha nyuma shule kongwe hapa nchini kama Mzumbe na Ilboru. 

Shule maarufu za Marian Girls na Boys mwaka huu zimefurushwa katika orodha hiyo. Shule ya  Wavulana ya Marian au Marian Boys imeporomoka kutoka nafasi ya sita kitaifa mwaka 2018  hadi nafasi ya 35 mwaka 2019 huku Shule ya Wasichana ya Marian ikishuka kutoka nafasi ya tisa mwaka 2018 hadi nafasi 17 mwaka 2019. 

Shule hizo zilizopo Bagamoyo mkoani Pwani zinaungana na shule kongwe ya umma za Mzumbe iliyopo Morogoro. 

Mwaka 2018 Shule ya Mzumbe ilishika nafasi ya nne kitaifa na sasa imeshika nafasi 13 kitaifa ikishuka kwa nafasi tisa wakati Shule ya  Wavulana ya Marian ikiporomoka nafasi 29. Shule ya Wasichana ya Marian au Marian Girls yenyewe imeshuka kwa nafasi nane. 

Shule ya Sekondari ya Illboru iliyopo mkoani Arusha ikishindwa kutoboa kwenye 10 bora baada ya kupanda  nafasi mbili kutoka nafasi 13 kitaifa mwaka 2018 hadi nafasi 11 kitaifa mwaka 2019. Wenzao Tabora Boys wamefanya maajabu baada kupanda kwa kasi kutoka nafasi 15 mwaka 2018 hadi nafasi 5 mwaka 2019.