October 6, 2024

Ngozi kuwavutia wawekezaji kutoka Misri

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji hao kuja nchini kwa sababu kuna malighafi nyingi ya ngozi.

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji hao kuja nchini kwa sababu  kuna malighafi nyingi ya ngozi. 
  • Amesema Serikaliimeboresha mazingira ya biashara pamoja na kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Dar es Salaam. Huenda wafugaji na wafanyabiashara wa ngozi wakafaidika na soko la Misri, baada ya Serikali kuanzisha juhudi za kuwashawishi wawekezaji wa nchi hiyo kuja Tanzania kuendeleza rasilimali ya ngozi inayopatikana kwa wingi. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali kutoka Misri ikiwemo kampuni ya Cairo for Investment and Development inayosimamia kiwanda cha ngozi cha Robbik waje kuwekeza nchini Tanzania.

Majaliwa aliyekuwa akizungumza jana (Julai 9, 2019) alipotembelea kiwanda hicho kilichopo katika mkoa wa Sharkia, Misri, amesema Tanzania ina malighafi nyingi ya ngozi ambayo inaweza kukidhi mahitaji ya kiwanda hicho. 

Waziri Mkuu ambaje jana alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi nchini Misri amesema Tanzania ina mifugo mingi hivyo inahitaji wawekezaji watakaojenga viwanda vya kuchakata bidhaa mbalimbali zitokanazo na mifugo ikiwemo ngozi.

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli imeboresha mazingira ya biashara na ya uwekezaji pamoja na kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hivyo Tanzania ni mahali bora na salama kwa wawekezaji na wafanyabiashara.


Soma zaidi: 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kampuni ya Cairo for Investment and Development, Yasser Mohamed Ahmed Al Maghraby amesema kiwanda hicho kinauhitaji mkubwa wa ngozi kutoka Tanzania.Amesema hiyo itakuwa fursa ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ngozi. Awali, Waziri Mkuu alitembelea mradi mkubwa wa mabwawa ya kufugia samaki, mradi wa upanuzi wa awamu ya pili ya mfereji wa Suez Canal, ambapo aliipongeza Serikali ya Misri kwa ujenzi wa mradi huo mkubwa kwa kutumia fedha za ndani. 

Katika hatua nyingine, Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Misri, Abdel Fattah Al- Sisi, ambapo wametumia fursa hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Misri.

Mbali na kuzungumzia masuala hayo ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na kijamii, pia Waziri Mkuu amemfikishia Rais wa Misri salamu kutoka kwa Rais John Magufuli.

Mazungumzo baina ya Waziri Mkuu na Rais wa Misri yamefanyika leo (Jumatano, Juni 10, 2019) Ikulu jijini Cairo, katika siku ya tatu na ya mwisho ya ziara yake ya kikazi nchini Misri. Katika ziara hiyo ameambatana na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga.