October 6, 2024

Watanzania wawekewa masharti mapya kuingia Norway

Ni maombi ya viza ambayo sasa yatakuwa yanashughulikiwa katika ubalozi wa nchi hiyo Nairobi nchini Kenya badala ya Tanzania.

  • Ni maombi ya viza ambayo sasa yatakuwa yanashughulikiwa katika ubalozi wa nchi hiyo Nairobi nchini Kenya badala ya Tanzania.
  • Watalazimika kulipa ada ya kusafirisha nyaraka za maombi ya viza  hadi Nairobi.
  • Watakaowasilisha maombi kabla ya Agosti 1, 2019 maombi yao yatashughulikiwa katika ubalozi wa Tanzania.

Dar es Salaam. Kama una mpango wa kusafiri kwenda nchini Norway katika siku za hivi karibuni, basi ubalozi wa nchi hiyo hapa Tanzania umeweka utaratibu mpya wa upatikanaji wa viza na vibali vya makazi kwa wageni wanaotaka kuingia katika nchi hiyo. 

Kuanzia Agosti 1 mwaka huu, Ubalozi wa Norway uliopo jijini Dar es Salaam hautahusika tena kushughulikia maombi ya viza au vibali vya makazi kwa wananchi waishio Tanzania. 

Badala yake maombi yatakayowasilishwa katika ubalozi huo, yatatumwa hadi katika Ubalozi wa Norway uliopo katika jiji la Nairobi, Kenya ambako ndiyo kituo cha kanda kinachoshughulikia masuala ya uhamiaji Afrika Mashariki.

Maombi yote yatakayosafirishwa hadi Nairobi yatafanyiwa kazi na kama muombaji amekidhi vigezo vyote atapatiwa kibali cha kuingia katika nchi hiyo iliyopo katika rasi ya Skandinavia. 

Taarifa ya ubalozi wa Norway nchini Tanzania iliyotolewa hivi karibuni, inaeleza kuwa kutokana na utaratibu huo mpya utakaoanza kutumika Agosti 1, utaambatana na mabadiliko kadhaa ambayo yanatakiwa kutimizwa na mwombaji wa viza au kibali cha makazi. 

Upokeaji wa maombi ya viza utaendelea kufanyika kwa kutumia mfumo uliopo unaosimamiwa na kampuni ya VFS Global Services na yatakuwa yanapokelewa katika kituo cha Dar es Salaam.  

“VFS Global itahakikisha kuwa maombi yote yanatumwa Nairobi kwa hatua zinafuata. Utakuwa na uwezo pia kukusanya pasipoti au nyaraka za maamuzi yako katika mfumo wa VFS Global,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. 


Zinazohusiana:


Lakini mwombaji atatakiwa kulipa ada ya kusafirisha kifurushi cha nyaraka za maombi hadi Nairobi pamoja ada ya maombi inayolipwa mtandaoni wakati wa usajili wa maombi ya viza. 

Kutokana na mabadiliko hayo, muda wa kusubiri kabla ya kupata viza nao utaongezeka ukilinganisha na ilivyozoeleka kwa siku 15 tangu maombi yanapowasilishwa. 

Utalazimika kusubiri kwa siku 2 hadi 4 zaidi ili kutoa muda wa kutuma nyaraka kutoka Dar es Salaam hadi Nairobi ambapo ni kama takribani siku 20 kabla ya kupata viza. 

“Tunashauri ufanye maombi mapema, japo wiki nne kabla ya mipango ya safari yako,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo. 

Hata hivyo, maombi ya viza ya Schengen inayotumika kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya (EU) yatakayofanywa kabla ya Agosti 1, 2019 yatashughulikiwa na kukamilishwa katika ubalozi wa Norway jijini Dar es Salaam. 

Lakini kama umefanya maombi ya kibali cha makazi kabla ya Agosti 1 mwaka huu, utataarifiwa kuhusu uamuzi wa maombi yako katika kituo cha VFS Global Dar es Salaam au ubalozi wa Norway nchini Kenya.