October 6, 2024

Tanzania itakavyonufaika na mahitaji ya kiuchumi ya SADC

Manufaa hayo yatafikiwa ikiwa itazingatia vipaumbele vya kujenga viwanda na upanuzi wa soko la bidhaa nje ya nchi.

  • Manufaa hayo yatafikiwa ikiwa itazingatia vipaumbele vya kujenga viwanda na upanuzi wa soko la bidhaa nje ya nchi.
  • Tanzania ikijipanga vizuri kimkakati inaweza kuwa ghala la chakula na soko la jumuiya hiyo.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu mstaafu Ofisi ya Waziri Mkuu, Mussa Uledi amesema Tanzania itaendelea kunufaika na fursa za kiuchumi katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwa itazingatia vipaumbele vya kujenga viwanda na upanuzi wa soko la bidhaa nje ya nchi.

Akizungumza leo (Julai 9, 2019) mjini Morogoro wakati akiwasilisha mada katika mafunzo ya Wanahabari kuripoti habari za SADC, Uledi amesema kuwa  Tanzania imenufaika na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya miundombinu,  biashara, uwekezaji  na viwanda ya jumuiya hiyo. 

“Mkakati wa maendeleo wa SADC unafafanana kwa kiwango kikubwa na ule wa Tanzania ambao pia unazingatia haja ya utekelezaji wa viwanda na miundombinu hapa nchini hali itakayochangia katika kuimarisha maendeleo na kukuza uchumi na ustawi wa wananchi,” amesema Uledi.

Amesema kuwa vipaumbele vya Tanzania vimejikita katika upanuzi wa mauzo nje na uongezaji wa michepuo yake, lengo likiwa ni kukuza na kuendeleza biashara hali inayowezesha uendelezaji wa viwanda vya kuongeza thamani kwa kutumia malighafi za ndani hususan mazao ya kilimo na madini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari-Maelezo, vipaumbele vingine kuwa ni pamoja na  uendelezaji miundombinu kama barabara, reli, usafiri wa anga, uzalishaji na usambazaji huduma za umeme ambayo ni nyenzo muhimu katika kuyaunganisha masoko ya nchi wanachama wa SADC.

Amesema Tanzania ikijipanga vizuri kimkakati inaweza kuwa ghala la chakula kwa kuongeza uzalishaji kuendana na mahitaji katika soko la jumuiya hiyo na hata nje ya jumuiya hiyo.


Soma zaidi:


Hivi karibuni, Rais John Magufuli alifanya ziara katika baadhi ya nchi za SADC ikiwemo Afrika Kusini na Namibia kabla ya kufanyika kwa mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo hapa nchini, Agosti mwaka huu.

Tanzania inatarajiwa kuleta msukumo mpya kwa nchi wanachama wa SADC katika utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo za jumuiya hiyo kwa kuwa itakuwa na dhamana kubwa ya kukidhi matarajio makubwa ya nchi wanachama wakati wote wa uenyekiti wake.

Kwa upande wake Mkuu wa Operesheni na Mafunzo, Brigedi ya Magharibi ya Jeshi  la Ulinzi la  Wananchi wa Tanzania (JWTZ),  Kanali Wilbert  Ibuge akizungumza katika mafunzo hayo amesema kuwa  Tanzania ni miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa barani Afrika zilizotoa mchango mkubwa na kuratibu kuanzishwa kwa mtengamano wa  SADC.

Amesema hali ya amani na usalama imeendelea kuimarika katika nchi za SADC na kutoa fursa ya kukuza uchumi, kuondoa umasikini na kuboresha hali ya maisha ya wananchi.

Msingi wa SADC ni kusimamia malengo yake ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii sambamba na yale ya ulinzi na usalama unaobainishwa katika Ibara ya 2 ya mkataba wa SADC ( Article 2 of SADC Treaty).