October 6, 2024

Maagizo matano ya Rais Magufuli kukuza utalii Tanzania

Ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kushughulikia changamoto ya gharama na usafi katika hoteli wanazofikia watalii.

  • Ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kushughulikia changamoto ya gharama na usafi katika hoteli wanazofikia watalii.
  • Kuweka mikakati ya kuwajengea uwezo waongozaji watalii na kuhakikisha wote wanatambuliwa rasmi.
  • Amewakaribisha wawekezaji kuwekeza katika sekta ya utalii ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametoa maagizo matano kwa Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuweka mikakati madhubuti ya kukuza sekta ya utalii Tanzania ikiwemo kushughulikia changamoto ya gharama na usafi katika hoteli wanazofikia watalii.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo (Julai 9, 2019) wakati akizindua hifadhi mpya ya Taifa ya Burigi Chato iliyopo Wilaya ya Chato mkoani Geita ambayo itakuwa ya tatu kwa ukubwa baada ya Ruaha na Serengeti.

Amesema pamoja na jitihada zinazofanyika na mafanikio yaliyopatikana, ni wazi kuwa bado mamlaka husika zinahitaji kuongeza bidii zaidi kuvutia watalii wengi ikizingatiwa kuwa Tanzania ina vivutio vingi vya utalii. 

“Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kujipanga vizuri na kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini,” amesema Rais Magufuli.

Ameitaka wizara hiyo kuanza kushughulikia malalamiko ambayo amekuwa akiyapata kupitia ripoti ya robo mwaka kutoka kwenye balozi za Tanzania ya baadhi ya watalii wanaolalamikia kuhusu gharama za utalii nchini kuwa ziko juu na changamoto za usafi kwenye hoteli. 

Pia ameitaka wizara hiyo inayoongozwa na Waziri Dk Hamis Kigwangalla kuwajengea uwezo waongazaji watalii na kuhakikisha wote wanatambuliwa rasmi ili kutoa huduma bora kwa watalii wanaoingia nchini.

“Hamna budi kufanyia kazi masuala haya na kufanya kaguzi mara kwa mara lakini pia wekeni mikakati ya kuwajengea uwezo waongozaji watalii na kuhakikisha wote wanatambuliwa rasmi,” amesisitiza. 


Zinazohusiana: 


Agizo lingine la kukuza utalii ambalo linatakiwa litekelezwe, ni kuhakikisha hifadhi za Taifa zinakuwa na mchanganyiko mzuri wa vivutio ikiwemo kuhamisha wanyama na mimea kutoka hifadhi moja kwenda nyingine ili kuhakikisha kunakuwa na uwiano mzuri wa vivutio hivyo. 

Rais amesema njia hiyo itasaidia kuokoa na kuendeleza maisha ya wanyama pindi magonjwa yanapolipuka katika eneo moja. 

“Naigiza Wizara kupanua wigo wa utalii nchini kwa kuongeza mazao ya utalii sambamba na utalii wa wanyama pori. Ingefaa iweke mkazo zaidi katika utalii wa fukwe na meli, utamaduni na kadharika,” amesema Rais. 

Aidha, wizara hiyo imetakiwa kushirikiana na mamlaka nyingine husika kuendelea kuboresha mazingira muafaka kwa ajili ya ukuaji wa sekta ya utalii ikiwemo kuendeleza mfumo wa kutoa huduma za pamoja za utalii ambao umesaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato ya wizara.

Katika hatua nyingine, Rais ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika sekta ya utalii kwa sababu Tanzania ina vivutio vingi. 

“Hata hapa Burigi-Chato kuna fursa nyingi za uwekezaji na hasa kwa kuwa iko karibu na Ziwa Victoria na ipo karibu na mto Kagera na hifadhi jirani ya Ikagera nchini Rwanda,” amesema. 

Awali hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato ambayo sasa imekuwa hifadhi ya ya 17 Tanzania, ilikua Pori la Akiba la Burigi kabla ya kupandishwa hadhi na kuwa hifadhi kamili.