October 6, 2024

Taboa wazungumzia agizo la Lugola kuruhusu mabasi kusafiri saa 24

Wamesema kutaleta tija kubwa na kupunguza gharama za uendeshaji kwa wamiliki wa mabasi.

  • Taboa yasema kilio chao cha muda mrefu kimesikilizwa.
  • Mabasi kusafiri msaa 24 kutapunguza gharama za uendeshaji na usumbufu kwa abiria.

Dar es Salaam. Chama Cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kimesema hatua ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kuruhusu mabasi kusafiri masaa 24 italeta  ahueni kubwa ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji hayo na usumbufu kwa abiria.

Waziri Lugola amepiga marufuku makamanda wa polisi wa mikoa nchini kuyazuia kusafiri usiku mabasi yanayotoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda Dar es Salaam kwa kisingizio cha kuhofia kuvamiwa na majambazi

“Mimi ndiyo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, hatuwezi kupangiwa ratiba ya kusafiri na majambazi, Serikali ya Rais (John) Magufuli ipo imara, na polisi ipo imara.

“Hivyo agizo hili ambalo pia niliwahi kulitoa lizingatiwe ipasavyo, niliagiza majambazi wote wasambaratishwe, asakwe mpaka jambazi wa mwisho, akamatwe kama kuku,” alisema Lugola katika mkutano wa hadhara jana,  katika Kijiji cha Namibu, Kata ya Neruma, Wilaya ya Bunda mkoani Mara

Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu ameiambia www.nukta.co.t kuwa wamepokea maagizo hayo kwa mikono miwli na wanapongeza agizo la Waziri Lugola kwa kuwa litaleta tija kubwa na kupunguza gharama za uendeshaji kwa wamiliki wa mabasi.

Amesema  agizo hilo la mabasi kutembea saa 24 katika baadhi ya njia kilikuwa kilo chao cha siku nyingi hivyo wanaamni limekuja muda mwafaka wakati ambao baadhi ya njia zinajaribiwa na kuona umakini wa madereva ili kuepukana na ajali.


Zinazohusiana:VTS: Vifaa vya kudhibiti ajali vinavyoogopwa na madereva waluwalu


“Ebu fikiria mfanyabishara mwenye mabasi mapya wa njia kama ya Mwanza ambaye alihitaji mabasi mawili moja la kwenda na lingine la kurudi  lakini kwa kulala njia ilibidi kuwa na mabasi zaidi ya mawili kwa njia moja, “ amesama Mrutu.

Amesema mfanyabiashara mwenye gari jipya ambaye gari lake linaweza kwenda hadi Mwanza kisha likafanyiwa matengenezo na kurudi Dar es Salaam siku inayofuata lakini kama likilala njiani inasababisha hasara kwa sababu linatumia siku mbili kufika mkoa husika.

“Fikiria kama gari hilo ilitakiwa kwenda Mwanza  na kurudi kesho yake na kuingiza mathalani Sh1.5 milioni kwa hiyo kama siku ambayo litalala njiani, mfanyabishara huyo atakosa hiyo milioni 1.5 ambayo ukifanya kwa mwezi ni hasara kubwa,” amesema Mrutu.

Ahueni nyingine itakuwa kwa abiria wanaosafiri kwa kutumia magari hayo, kwa sababu walikuwa wanalazimika kulala njiani, jambo lililokuwa linawaongezea gharama za chakula na wengine kulala kwenye nyumba za kulala wageni wakisubiri siku inayofuata kuendelea na safari. 

Julai 17, 2018, akiwa katika ziara Makao Makuu ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Ukonga, Dar es Salaam, Kangi alimpa siku 14, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kuhakikisha biashara zinafanyika kwa saa 24 ikiwamo mabasi kusafiri muda wote

“Tunataka Watanzania wafanye kazi za kiuchumi kwa saa 24. Hatuwezi tukafikia malengo ya uchumi wa kati kama Watanzania hawafanyi shughuli za kiuchumi,” alisema Lugola.