November 24, 2024

Ujenzi wa makazi ya kisasa wapaa Tanzania

Kaya 8 kati ya 10 zimejenga makazi yao kwa kutumia njia za kisasa, hali ikiwa bora zaidi ikilinganishwa na miaka sita iliyopita.

  • Ujenzi wa makazi kwa kutumia vifaa vya kisasa waongezeka mara  1.7 ndani ya miaka sita iliyopita.
  • Licha ya ukuaji huo, bado robo ya makazi vijijini hayajajengwa kwa kutumia vifaa vya kisasa.  

Dar es Salaam.Ujenzi wa makazi bora kwa kutumia vifaa vya kisasa hususan paa za nyumba,kuta na sakafu Tanzania umeongezeka kwa zaidi ya mara 1.7 ndani  ya miaka sita iliyopita.

Ripoti mpya ya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya  mwaka 2017/18 iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Ofisi ya  Taifa ya Takwimu (NBS) imebainishauwepo wa ongezeko kubwa  la kaya Tanzania Bara zinazotumia  vifaa vya kisasa kwenye ujenzi wa makazi hasa kwenye mapaa, ukuta na sakafu umeongezeka kutoka asilimia 46 mwaka 2011-2012 hadi asilimia 79 mwaka 2017-18.

Ongezeko hilo ni sawa na kusema takriban kaya 8 kati ya 10 kwa sasa zimetumia vifaa ya kisasa katika ujenzi wa nyumba zao ukilinganisha na kaya takribani 5 kati ya 10 zilizokuwa hatua hiyo mwaka 2011-2012.


Yanayohusiana:


Ripoti hiyo imebainisha kuwa idadi ya kaya zinazojenga makazi yao kwa kutumia paa za kisasa zimefikia asilimia 84.1 ikiwa ni sawa na kaya 84 kwa kila 100 zilizopo Tanzania Bara. Paa za kisasa ni pamoja ujenzi wa bati na vigae. 

Ukiacha na paa ambalo ni muhimu kusitiri wakazi wa kaya husika na adha ya mvua na jua, ujenzi wa kuta za kisasa nao umekua kwa kasi ndani ya miaka ya hivi karibuni hadi asilimia 79 mwaka 2017/18 kutoka asilimia 46 iliyorekodiwa mwaka 2011/12. Hii ina maana kuwa idadi ya kaya nchini zilizojenga nyumba zao kwa kuta za vifaa vya kisasa yakiwemo matofali ya kuchoma na saruji imeongezeka zaidi ya mara moja ya nusu kutoka kaya 46 kati ya 100 mwaka 2011/12 hadi kaya 79 kati ya 100 mwaka 2017/18. 

Katika kipindi hicho cha miaka sita iliyopita, pia zipo kaya zilizojiongeza kwa kuimarisha sakafu za nyumba zao. Ripoti hiyo inabainisha kuwa kwa sasa nusu ya kaya zote Tanzania Bara (asilimia 50.1)i zimejenga nyumba zao kwa sakafgu za kisasa kutoka kaya nne kati ya 10 (asilimia 40) zilizokuwapo mwaka 2011/12. 

Ukiachilia ukuaji huo wa jumla kwa upande wa vijijini kaya zinazojenga kwa kutumia vifaa za kisasa zimekuwa ni ndogo hususani kwenye ujenzi wa  sakafu za kisasa ukilinganisha na zile za mijini. 

Robo tatu au kaya 76 kati ya kaya 100 za vijijini ziliweza kujenga kwa kutumia paa za kisasa licha ya ukweli kuwa baadhi ya hivyo vya kisasa huwa ni ghali kuvifikisha katika maeneo hayo yenye changamoto lukuki za miundumbinu.

Katika maeneo hayo ya vijijini ripoti hiyo imebainisha kuwa kaya takriban 71 kati ya 100 zimejenga nyumba zao kwa kuta bora wakati theluthi moja tu zimefanikiwa kuweka sakafu za kisasa katika makazi yao.

Tofauti na vijijini, wakazi wa mijini kwa sehemu kubwa makazi yao yamejengwa na njia za kisasa baada ya utafiti huo kubainisha kuwa karibu kaya zote nyumba zao ziliezekwa kwa paa za kisasa ikiwa ni asilimia 98. 

Katika kaya hizo za mijini zikiwemo za majiji makubwa ya Dar es salaam, Mwanza na Mbeya, ujenzi wa kuta za kisasa nao ni wa juu baada ya utafiti huo uliofanywa na NBS kubainisha kuwa kaya 94 kati ya 100 zilizopo katika maeneo hayo nyumba zimejengwa kwa kuta za kisasa ikiwemo kutumia matofali ya saruji.