November 24, 2024

Hii ndiyo tofauti ya uunganishwaji umeme katika kaya Tanzania

Tofauti hiyo inajitokeza hasa katika maeneo ya mijini ambayo kaya zake zimeunganishwa kwa asilimia 63.2 na huku vijijini ikiwa ni asilimia 29.1.

  • Kaya  nyingi za vijijini bado hazijaunganishwa na umeme ukilinganisha na mijini.
  • Pia tofauti kubwa inajitokeza katika mikoa huku Dar es Salaam ukiongoza kwa kuwa na kaya nyingi zenye umeme.
  • Serikali yasema inaendelea na jitihada za kuupeleka umeme vijijini ili kupunguza pengo.

Dar es Salaam. Licha ya juhudi za Serikali kupeleka umeme vijijini, bado kaya nyingi za maeneo hayo hazijaunganishwa na nishati hiyo ambayo ni muhimu katika shughuli za nyumbani na uzalishaji. 

Ripoti mpya ya mapato na matumizi ya kaya mwaka 2017/18 iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa asilimia 10.4 au kaya moja kati ya 10 ndiyo imeunganishwa na umeme katika maeneo ya vijijini.

Uunganishwaji huo wa umeme uko chini ya wastani wa kitaifa ambao asilimia 29.1 ya kaya zote za Tanzania Bara zimeunganishwa na umeme ikiwa na ongezeko la asilimia 11.1 ukilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2011/2012.

Wakati kaya za vijijini zikiwa chini ya wastani wa kitaifa, kaya za mjini hadi kufikia mwaka 2017/2018 zilikuwa zimeunganishwa na umeme kwa asilimia 63.2 na kuvuka wastani wa kitaifa kwa zaidi ya mara mbili. Hii ni ina maana kuwa takriban kaya mbili kati ya tatu za mijini zimeunganishwa na nishati hiyo.

Tofauti hiyo ya uunganishwaji wa umeme katika maeneo ya mijini na vijijini pia inajihirisha kati ya mkoa na mkoa ambapo bado kuna tofauti kubwa ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu ya nishati. 

Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo kinara wa kuwa na kaya nyingi zilizounganishwa na umeme ambapo kwa kila kaya 100, basi 80 zimeungwanishwa na umeme katika jiji hilo, linalokua kwa kasi Afrika Mashariki

Jiji hilo linafuatiwa kwa mbali na mkoa wa Kilimanjaro ambao kwa kila kaya 100 basi 44 zina umeme na Mbeya ni 33 kati ya 100.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa mkoa wa Singida ndiyo wenye kaya chache zilizounganishwa na umeme ambapo ni kaya 75 tu kwa kila kaya 1,000 ndiyo zina umeme. 


Soma zaidi:


Hata hivyo, kutokana na umeme wa gridi kutokidhi mahitaji ya wananchi wote wa Tanzania hasa vijijini, kampuni mbalimbali zinaendelea kusambaza nishati jadidifu ikiwemo umemejua ambao unatajwa kuwa rafiki wa mazingira na endelevu.

Kampuni hizo ni pamoja na Zola, Ensol na Power Corner ambazo zimejikita zaidi kusambaza vifaa vya sola na kuwaunganishia wananchi wa vijijini umemejua katika nyumba na biashara zao.

Aidha, Serikali imesema katika utekelezaji wa bajeti ya 2019/2020 inakusudia kuongeza wigo wa upatikanaji wa nishati ikiwa ni miongoni mwa hatua za uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji nchini. 

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, wakati akiwasilisha bajeti hiyo mbele ya Bunge alisema hadi kufikia Aprili 2019, kiasi cha Sh269.3 bilioni kimetolewa na Serikali kwa ajili ya awamu ya tatu ya mradi wa kupeleka umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).