November 24, 2024

Mapato sekta ndogo ya wanyamapori yapaa

Mapato hayo yameongezeka kwa asilimia 15.1 hadi kufikia Sh34.3 milioni mwaka jana kutoka Sh29.7 milioni mwaka 2017.

Jitihada mbalimbali za kuiboresha na kuikuza sekta ndogo ya wanyamapori zinaendelea ikiwemo kuunda kikosi kazi cha kulinda maliasili zilizopo nchini. Picha|Mtandao.


  • Mapato hayo yameongezeka kwa asilimia 15.1 hadi kufikia Sh34.3 milioni mwaka jana kutoka Sh29.7 milioni mwaka 2017.
  • Kuimarika kwa doria na mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato (GePG) wachangia kuongezeka kwa mapato hayo. 
  • Uanzishwaji wa mfumo wa Jeshi Usu kuwahakikishia usalama wanyamapori.

Dar es Salaam. Kuimarika kwa doria na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato (GePG) kumechangia mapato ya sekta ndogo ya wanyamapori kuongezeka kwa asilimia 15. 1 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita. 

Wanyamapori ni msingi wa utalii wa kupiga picha na uwindaji ambapo imekuwa rasilimali muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania. 

Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kinaeleza kuwa mwaka 2018, sekta ndogo ya wanyamapori ilikusanya Sh34.3 milioni ikilinganishwa Sh29.7 milioni  zilizokusanywa mwaka 2017. 

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 15.1 katika kipindi cha mwaka mmoja. 

“Ongezeko hilo lilitokana na utumiaji wa mfumo wa kielektroniki wa kukusanya mapato (GePG) katika sekta ndogo ya wanyamapori,” inasomeka sehemu ya kitabu hicho. 

Ukuaji wa mapato ulichangiwa pia na kuimarika kwa doria  maeneo yaliyohifadhiwa, hifadhi za Taifa, mapori ya akiba na mapori tengufu ili kudhibiti ujangili na uvamizi wa wananchi. 

Katika doria hizo, vitu na nyara mbalimbali za wanyamapori zilikamatwa ikiwa ni pamoja na meno ya tembo mazima 413 na vipande 211; bunduki 469; na risasi za aina mbalimbali 386. 

“Kufanyika kwa doria hizo kulipunguza idadi ya matukio ya uhalifu ukiwemo ujangili wa tembo kwa wastani wa asilimia 50 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita,” kinaeleza kitabu hicho ambacho kilitolewa Juni mwaka huu. 


Zinazohusiana:


Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii, sensa iliyofanyika mwaka 2018 katika mfumo wa ikolojia wa Selous-Mikumi, idadi ya tembo ilikuwa takribani 15,500 kama ilivyokuwa katika Sensa ya mwaka 2015. 

Hata hivyo, jitihada mbalimbali za kuiboresha na kuikuza sekta ndogo ya wanyamapori zinaendelea ikiwemo kuunda kikosi kazi cha kulinda maliasili zilizopo nchini. 

Mwaka 2018, Serikali iliendelea kukamilisha uanzishwaji wa mfumo wa Jeshi Usu unaojumuisha idara za wanyamapori, misitu na nyuki na taasisi za Mamlaka ya Hifadhi za Taifa, Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Wakala wa Huduma za Misitu na Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori ili kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa maliasili. 

“Aidha, watumishi 2,176 kutoka taasisi hizo walipatiwa mafunzo ya kijeshi. Vile vile, marekebisho ya sheria zilizo chini ya sekta ya wanyamapori na misitu yanaendelea ili kuwezesha utekelezaji wa mfumo wa Jeshi Usu,” kinaeleza kitabu hicho.