Bunge lapitisha bajeti ya 2019-20 licha ya upinzani mkali wa Pedi Bila Kodi
Bajeti hiyo ya Serikali kwa mwaka 2019/20 ya Sh33.1 trilioni imepitishwa baada ya zaidi ya robo tatu ya wabunge waliokuwepo bungeni leo kupigia kura ya “Ndiyo”.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto) akizungumza na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kabla ya upitishaji wa Bajeti Kuu ya Serikali iliyojadiliwa kwa siku saba kwa kupitisha Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali mwaka 2019. Picha|Mtandao.
- Bajeti hiyo ya Serikali kwa mwaka 2019/20 ya Sh33.1 trilioni imepitishwa baada ya zaidi ya robo tatu ya wabunge waliokuwepo bungeni leo kupigia kura ya “Ndiyo”.
- Hii ni sawa na kusema wabunge wanane kati ya 10 waliokuwepo bungeni leo waliridhia bajeti hiyo kupita
Dar es Salaam. Bunge limepitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2019/20 ya Sh33.1 trilioni baada ya zaidi ya robo tatu ya wabunge waliokuwepo bungeni leo kuipigia kura ya “Ndiyo”.
Bajeti hiyo ya Serikali imepitishwa licha ya kuwepo upinzani mkali kutoka kwa wanaharakati na baadhi ya wabunge juu ya uamuzi wa Serikali wa kurejesha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo za kike.
Upitishaji huo wa bajeti hiyo iliyojadiliwa kwa siku saba umehitimishwa leo kwa kupitisha Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali mwaka 2019 (The Appropriation Bill Act, 2019).
Spika wa Bunge, Job Ndugai ameliambia Bunge kuwa asilimia 78.2 ya wabunge waliokuwepo bungeni jioni ya leo (25 Juni 2019) wamepiga kura ya “Ndiyo” na kuwabwaga wenzao waliopinga bajeti hiyo kwa kupigia kura ya “Hapana” ambao walikuwa asilimia 21.8.
“Kwahiyo natangaza rasmi kabisa kwa kura hizi asilimia 78.2 kwamba Bunge rasmi limekubali kupitisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/20,” amesema Ndugai huku akifuatiwa na shangwe za baadhi ya wabunge waliokuwa wakipiga makofi na kugonga meza.
Hii ni sawa na kusema wabunge wanane kati ya 10 waliokuwepo bungeni leo wameridhia bajeti hiyo kupita ambayo miongoni mwa mambo mengine imefuta tozo 54 zilizokuwa zinachangia kukwamisha ufanyaji wa biashara nchini.
Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai aliyekuwa akieleza taarifa za kina za upigaji kura huo ameeleza kuwa jioni ya leo kulikuwa na wabunge 380 walioshiriki kupiga kura kupitisha bajeti hiyo huku 12 wakiwa hawapo kutokana na sababu mbalimbali. Bunge lina wabunge 393 akiwemo Spika Ndugai.
Zinazohusiana:
- Serikali yasema ongezeko la bajeti ya kilimo litategemea mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine
- Serikali yaanika bajeti ya mwaka 2019/2020
- Dk Mpango-Wastani wa pato la kila mtu waongezeka Tanzania
Licha ya kufanya maboresho katika sehemu ya kodi na tozo ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara, bado wadau mbalimbali wameilalamikia Serikali kwa uamuzi wake wa kufuta msamaha wa VAT kwenye taulo za kike iliyoutoa katika mwaka wa fedha unaoisha mwezi huu kwa sababu haukuwanufaisha walengwa ambao ni watoto wa kike na wanawake.
Leo katika kujibu hoja za wabunge kuhusu jambo hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ameendelea kusisitiza kuwa kodi hiyo haikuwasaidia walengwa na kwamba dhamira ya Serikali ni njema kwa kuwa kodi ina mchango mdogo kwenye bei ya mwisho ya bidhaa hiyo.
Amesema Serikali inazingatia afya ya mwanamke na imeshatoa fedha nyingi katika kuboresha mazingira ya utoaji huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini.
“Serikali ya Chama cha Mapinduzi inamjali sana mwanamke. Mwanamke wa Tanzania akiwa vijijini ndiye anayelilisha Taifa hili…na mimi nikajiuliza huyu mwanamke anayelilisha Taifa anashindwa kuwa na Sh3,000 kwa ajili ya kununua taulo ya kike?,” amesema Dk Kijaji wakati akijibu hoja za wabunge.
Amesema kuwa wanawake wengi walikuwa hawajui kuwa kodi ilikuwa imeondolewa na waligundua kuwa bei hajaipungua kwa mlaji wa mwisho na viwanda vya ndani vilikuwa vimepunguza uzalishaji kutokana na msamaha wa kodi hiyo.
Amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kuendelea kuondoa ushuru wa forodha wa asilimia 10 kwa malighafi zote zinazotumika katika kutengeneza taulo za kike ambayo ilishaondolewa tangu mwaka 2012 na ujenzi wa viwanda vya kuzalisha taulo za kike kupitia ubia na sekta binafsi (PPP), jambo litakalokuwa ni rahisi kudhibiti bei.