October 6, 2024

Rais Magufuli ataka Serikali kutojiingiza sana uwekezaji sekta binafsi

Amewataka wajikite kukusanya mapato na kuweka utaratibu mzuri wa wawekezaji kufanya shughuli zao.

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Juni 25, 2019) wakati akizindua ghala na mitambo ya kuchakata gesi ya majumbani (LPG) iliyoko wilayani ya Kigamboni, Jijini Dar es Salaam. Picha|Mtandao.


  • Amewataka wajikite kukusanya mapato na kuweka utaratibu mzuri wa wawekezaji kufanya shughuli zao.
  • Wametakiwa kuzungumza na wawekezaji kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.
  • Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara ili kuvutia wawekezaji.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewataka watendaji wa Serikali kutojiingiza na kudhibiti  uwekezaji katika sekta binafsi bali wajikite katika kukusanya mapato na kuweka utaratibu mzuri utakaozifaidisha pande zote mbili. 

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Juni 25, 2019) wakati akizindua ghala na mitambo ya kuchakata gesi ya majumbani (LPG) iliyoko wilayani ya Kigamboni, Jijini Dar es Salaam, amesema wakati mwingine upande wa Serikali umekuwa unakimbilia kudhibiti sekta binafsi lakini baadaye unaharibu maana nzima ya uwekezaji.

“Wizara (Wizara ya Nishati) na wawekezaji ni vyema mkakaa na mkakubaliana katika taratibu nzuri za  ‘win win situation’ (maslahi ya pande zote) kwa sababu saa nyingine upande wa Serikali tunakimbilia sana kukusanya na kujifanya tunaweza kudhibiti halafu baadaye tunaharibu,” amesema. 

Agizo hilo la Rais linakuja baada ya Wizara ya Nishati kuandaa mpango wa pamoja wa uagizaji wa gesi ya mitungi (LPG) ili kudhibiti usambazaji na bei elekezi ya gesi hiyo inayotumika zaidi katika shughuli za nyumbani. 

Hata hivyo, Rais amesema hakuwa na taarifa na mpango huo mpya lakini Serikali na wawekezaji wakae pamoja kuangalia namna ya kupata haki kwa usawa kupitia uagizaji huo.

“Ninachotaka kusema ni kwamba ninyi wote mzungumze ili kusudi Serikali ipate haki yake iliyo ya haki, lakini Serikali nayo isijiingize sana kwenye uwekezaji wa sekta binafsi kwa sababu walishindwa Serikali kuleta hii gesi.

“Mnakimbia haraka haraka kufanya nini, badala ya kukaa na kukusanya revenue (mapato), kwa hiyo mambo haya yote tuyaangalie kwa pamoja,” amesema Rais Magufuli.


Soma zaidi:


Hata hivyo, amesema wataendelea kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara na uzalishaji wa nishati ya umeme wa kutosha ili kuvutia wawekezaji kufanya biashara zao kwa uhuru. 

“Bei ya umeme kwa Watanzania na wawekezaji tutaishusha ili wawekezaji wengi waweze kupata faida katika miradi yao watakayokuja kuwekeza katika nchi hii,” amesema Rais.