October 6, 2024

Serikali yavuna gawio jingine la Sh7 bilioni kutoka CRDB

Gawio hilo linatokana na uwekezaji wa asilimia 21 ya hisa katika benki hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

  • Gawio hilo linatokana na uwekezaji wa asilimia 21 ya hisa katika benki hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
  • Mwenyekiti wa CRDB abainisha kuwa benki hiyo ilipata faida ya Sh64.1 bilioni baada ya kodi mwaka 2018 ikilinganishwa na faida ya Sh36.2 bilioni iliyopatikana mwaka 2017.

Dar es Salaam. Wiki tatu baada ya kupokea gawio la Sh2.1 bilioni kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Serikali imepokea gawio jingine kutoka benki ya biashara ya CRDB PLC la Sh6.8 bilioni baada ya benki hiyo kupata faida mwaka 2018.

Taarifa ya Wizara ya Fedha na Mipango iliyotolewa leo (Juni 15, 2019) inaeleza kuwa gawio hilo linatokana na uwekezaji wa asilimia 21 ya hisa katika benki hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Gawio hilo ni sehemu ya Sh10 bilioni ambazo benki hiyo imetoa kama gawio kwa mashirika na taasisi mbalimbali za umma zenye hisa katika benki hiyo, taarifa hiyo imeeleza.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amepokea gawio hilo kwa niaba ya Serikali na kukabidhi baadhi ya mashirika na taasisi za umma zilizopata gawio kutoka benki hiyo wakati wa hafla ya makabidhiano ya mfano wa hundi za gawio hilo iliyofanyika jijini Dodoma.

Dk Mpango ameupongeza uongozi wa benki hiyo kwa kurudisha fadhila kwa mwananchi na kuzitaka benki na taasisi zote za fedha nchini kuiga mfano wa benki hiyo kwa maendeleo ya nchi.

“Benki ya CRDB na benki zingine muongeze jitihada ili kuongeza gawio kwa Serikali ili iweze kuwahudumia wanachi katika huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na maji,” ameeleza Dk Mpango.

Amezitaka benki na taasisi za fedha kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa huduma za benki ili waweze kujikomboa kiuchumi na kuiwezesha nchi kupata gawio kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo.


Soma zaidi: 


Mei 21 mwaka huu Rais John Magufuli alipokea gawio la Sh2.1 bilioni kutoka TTCL baada ya kupata faida mwaka 2018. Gawio hilo lilipanda kwa Sh600 milioni kutoka Sh1.5 bilioni lililotolewa mwaka jana.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Ally Laay amesema mwaka 2018 benki hiyo ilipata faida ya Sh64.1 bilioni baada ya kodi ikilinganishwa na faida ya Sh36.2 bilioni iliyopatikana mwaka 2017.

Amesema sehemu ya mafanikio hayo yamechagizwa na matumizi ya mfumo wa Serikali wa malipo kwa njia ya kielektroniki (GePG).

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema benki hiyo imewekeza fedha kwenye mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji katika mto Rufiji mkoani Pwani na kwamba benki yake iko tayari kuwekeza kwenye ujenzi wa miradi mingine ukiwemo ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa (SGR).

Taarifa hiyo ya wizara ya fedha imeeleza kuwa miongoni mwa mashirika na taasisi za umma zilizopokea gawio ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma-PSSSF (Sh2.4 bilioni), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya-NHIF (Sh243.5 milioni), Mfuko wa Hifadhi ya Taifa-NSSF (Sh111.5 milioni) na Mfuko wa Mafao kwa Wafanyakazi wa Serikali-GEPF (Sh56.7).

Waziri wa Fedha na Mipango,Dk Philip Mpango (katikati) akiwa ameshika hundi kifani aliyoipokea kama gawio la Serikali kutoka Benki ya CRDB. Kutoka kushoto ni Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Einar Jensen,  Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Ally Laay na Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Khatibu Kazungu na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Abdulmajid Nsekela katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma. Picha|Wizara ya Fedha na Mipango.