Serikali ya Tanzania yaanika vipaumbele vinne bajeti 2019-2020
Imesema bajeti hiyo itajikita kuboresha kilimo na uanzishwaji wa viwanda vinavyotumia malighafi za ndani na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema vipaumbele hivyo kwa mwaka 2019/20 ambavyo vitatekelezwa kwa kuzingatia umuhimu wa pekee wa kulinda mazingira nchini. Picha|Mtandao.
- Imesema bajeti hiyo itajikita kuboresha kilimo na uanzishwaji wa viwanda vinavyotumia malighafi za ndani.
- Pia itaboresha mazingira ya biashara na uwekezaji sambamba na uimarishaji wa mfumo wa ukusanyaji kodi.
Dar es Salaam. Serikali imeanisha vipaumbele vikuu vinne inavyokusudia kutekeleza katika mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwemo uboreshaji wa mazingira wezeshi ya ufanyaji wa biashara ili kuvutia wawekezaji na kuongeza mapato ya Serikali yatokanayo na kodi na yasiyo ya kodi.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliyekuwa akizungumza Bungeni leo (Juni 13, 2019) wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali Kuu kwa mwaka 2019/2020, amesema vipaumbele hivyo vitawezesha katika utekelezaji wa sera za uchumi wa viwanda na kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Amesema kipaumbele cha kwanza ni viwanda na kilimo ambapo katika kuendeleza azma ya uchumi wa viwanda katika mwaka 2019/2020 Serikali itajikita zaidi kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vinavyotumia malighafi za ndani kama vile mazao na mifugo.
Kipaumbele kingine ni ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa kuimarisha utoaji wa huduma bora za kijamii ikiwemo elimu na afya ili kuimarisha nguvukazi ya Watanzania kuwawezesha kutimiza majukumu ya ujenzi wa uchumi na shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Bajeti ya 2019/2020 itaelekezwa kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, ujuzi, chakula, lishe bora na maji safi na salama. Aidha, katika bajeti hii msukumo utawekwa katika kuongeza ubora wa nguvukazi ili iendane na mahitaji ya soko la ajira,” amesema Dk Mpango. .
Lakini nguvu pia itaelekezwa katika uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa ajili ya uendeshaji wa biashara ambapo bajeti hiyo itakayoanza kutekelezwa Julai 1 mwaka huu imeweka msisitizo mkubwa katika ujenzi na kuendeleza miundombinu hususani reli, bandari, nishati, barabara, madaraja na viwanja vya ndege.
Miundombinu hiyo itasaidia kuwavutia wawekezaji kuyafikia maeneo mbalimbali ya uwekezaji kwa urahisi na kutumia rasiliamli zilizopo nchini kwa ajili ya manufaa ya wananchi na Taifa.
“Kuanzia mwaka ujao wa fedha, Serikali itaanza kutekeleza kwa nguvu zaidi mpango kazi wa kuboresha mazingira ya biashara ili mazingira ya biashara nchini kwetu yawe rafiki zaidi na yenye gharama nafuu,” amesema Waziri huyo.
Soma zaidi:
- Dk Mpango – Wastani wa pato la kila mtu waongezeka Tanzania
- Serikali kulenga shabaha tano za uchumi mwaka 2019-2020
Katika hatua nyingine, Serikali inakusudia kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi zote ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji unakuwepo katika ofisi za umma zinazotoa huduma muhimu kwa wananchi.
Aidha, Serikali imebainisha kuwa itaimarisha ukusanyaji wa mapato yote ya kodi na yasiyo ya kodi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa bajeti na kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unafanyika bila kuathiri biashara.
“Napenda kuwasisitiza tena watumishi wa TRA kwamba hairuhusiwi kufunga biashara ili kushinikiza mfanyabiashara alipe kodi au malimbikizo ya kodi isipokuwa kwa kibali cha Kamishna Mkuu wa TRA,” amesisitiza Waziri huyo.
Vipaumbele hivyo kwa mwaka 2019/20 ambavyo vitatekelezwa kwa kuzingatia umuhimu wa pekee wa kulinda mazingira nchini (environmental sustainability).