October 6, 2024

Waziri Kigwangalla awapa kibali wananchi kujenga shule ndani ya hifadhi ya Ngorongoro

Ni wananchi wa kata ya Alaitole wilayani Ngorongoro ambao walizuiwa kwa muda mrefu kutekeleza ujenzi huo kutokana na mgogoro uliokuwepo na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

  • Ni wananchi wa kata ya Alaitole wilayani Ngorongoro ambao walizuiwa kwa muda mrefu kutekeleza ujenzi huo.
  • Sh298 milioni zilizotolewa na Serikali ili kukamilisha shule hiyo ya sekondari ya bweni. 
  • Ngorongoro ni hifadhi mseto inayoruhusu binadamu na wanyama kuwepo katika eneo moja.
  • Dk Kigwangalla autaka uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuanza kutumia nguvu kutatua migogoro na wananchi.

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro uwaruhusu wananchi wa kata ya Alaitole wilayani Ngorongoro wajenge  shule ya wasichana ya bweni katika eneo la Esere lililo ndani ya mamlaka hiyo, ili wapate elimu kufuatia wananchi hao kuzuiwa kwa muda mrefu kutekeleza ujenzi huo.

Dk Kigwangalla ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo jana (Juni 10, 2019) kwenye mkutano wa hadhara.  

Ameutaka uongozi wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro utoe kibali cha kuwawezesha wananchi kata hiyo kuanza ujenzi haraka iwezekanavyo ili fedha kiasi cha Sh298 milioni zilizotolewa na Serikali zitumike.

“Jambo hili ninalifunga rasmi, shule itajengwa pale eneo lisizidi ekari 15 ili shule hii ijengwe karibu na shule yenu ya msingi ili watoto wapate fursa ya kusoma,” amesema Dk Kigwangalla.

Amesema Serikali inaunga mkono juhudi zote za wananchi za kujiletea maendeleo akifafanua kuwa hatua ya wananchi hao kuamua kujenga shule ya sekondari ya bweni ni jambo  linalopaswa kupongezwa na kila mpenda maendeleo.

Waziri huyo amesema kuwa ujenzi wa shule hiyo utawaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu na kuwafanya watulie sehemu moja ili kupata elimu bora.


Zinazohusiana:


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Ngorongoro ni hifadhi mseto inayoruhusu binadamu na wanyama kuwepo katika eneo moja.

Katika hatua nyingine, ameutaka uongozi wa Mamlaka hiyo uendelee kufanya mazungumzo na wananchi hao badala ya kujielekeza katika matumizi ya nguvu ili kupata uelewa wa pamoja akitolea mfano wa eneo la Loliondo ambalo hivi sasa lina utulivu.

“Viongozi wa Mamlaka mnalo jukumu la kuwasikiliza wananchi na kuamua kwa pamoja, eneo la Ngorongoro lina thamani ya kipekee ni urithi wa dunia lakini pamoja na uthamani wake kitaifa na Kimataifa haiondoi uthamani wa wananchi wetu wanaoishi hapa katika eneo hili. 

“Hapa ni kwao walipozaliwa wamezika babu, baba zao na watoto wao ni lazima tujifunze kuheshimu na kuthamini maslahi  ya walio wengi,” amesisitiza Dk Kigwangalla.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamis Kigwangalla (kushoto) akisikiliza maoni na hoja za wananchi wa kata ya Alaitole alipofika kutatua mgogoro wa wananchi wa kata hiyo kuzuiwa kujenga shule ya wasichana ya bweni na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro  katika eneo lao la Esere, wilayani Ngorongoro jijini Arusha. Picha|Wizara ya Maliasili na Utalii.

Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ngorongoro, William Ole Nasha akizungumza wakati wa mkutano huo amempongeza na kumshukuru Waziri Kigwangalla kwa kuwapa kibali wananchi kujenga shule katika eneo hilo.

Amesema maridhiano hayo ni ishara tosha kwamba Serikali inawalinda na kuwajali wananchi wake.

Kwa upande wao wananchi wa kata ya Alaitole wamemshukuru Dk Kigwangalla kwa kuzungumza nao katika makazi yao wakimpongeza kwa juhudi zake za kutatua changamoto mbalimbali kwa maslahi ya wananchi na uhifadhi.

Aidha, wamemwomba kuendelea kuisimamia sekta ya uhifadhi nchi wakitoa wito wa kudumisha mahusiano mema baina ya wananchi na wahifadhi.