November 24, 2024

Magufuli asema wawekezaji Bandari ya Bagamoyo wana masharti ya ajabu

Baadhi ta masharti hayo ni kuwa Serikali haitaruhusiwa kuendeleza bandari yeyote ukanda wa pwani na hautoruhusiwa kukusanya mapato.

Rais John Magufuli akizungumza na wafanyabiashara leo katika mkutano uliofanyika Ikulu. Picha|Mtandao.


  • Rais Magufuli amesema wawekezaji hao wanataka wasilipe kodi na wapewe mkataba wa kumiliki ardhi miaka 99 kinyume na sheria.
  • Amesema ni kichaa tu anaweza kukubali masharti hayo “ya ajabu”.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema wawekezaji wa bandari ya Bagamoyo wamependekeza masharti magumu ambayo ni vigumu kwa Serikali kuyatekeleza na “kichaa tu ataweza kuyakubali masharti hayo.”

Dk Magufuli amewaambia wafanyabiashara leo (7 Juni 2019) katika mkutano uliofanyika Ikulu kuwa wawekezaji hao wanataka mara baada ya kujengwa bandari hiyo itakayogharimu Dola za Marekani 10 bilioni (Sh22.7 trilioni) Serikali haitaruhusiwa kuendeleza bandari yoyote kutoka Tanga hadi Mtwara.

Wawekezaji China Merchants Holding International and State General Reserve of Oman ndiyo wanaowekeza katika ujenzi wa bandari hiyo ambayo ni sehemu ya eneo maalumu la uwekezaji wa kiuchumi la Bagamoyo.

“Wawekezaji hawa wanakuja na masharti ya ajabu na ni kichaa tu anaweza kuyakubali,” amesema Rais Magufuli akionyeshwa kukerwa na masharti hayo.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema baada ya kuwekeza katika bandari hiyo, wawekezaji wanataka Serikali isichukue mapato yote kutoka kwenye mradi huo huku akichagiza kuwa “hata TRA hairuhusiwi kukanyaga pale wakishafanya ‘investment’ (uwekezaji)”.

“Unatakiwa uwape guarantee (dhamana) ya kwanza bila hata kuulizwa kwa miaka 33. Unatakiwa uwape lease (mkataba wa kumiliki wa ardhi) tofauti na sheria za nchi ‘for 99 years’ (kwa miaka 99) na huruhusiwi hata kwenda kumuuliza atakayekwenda kuwekeza pale na wao wawe na mandate (mamlaka)ya kuchukua hilo eneo kama ardhi yao,” amesema Rais Magufuli.


Soma zaidi: 


Pamoja na yote hayo, Dk Magufuli amesema wawekezaji wanataka kupewa fidia ya gharama za uchimbaji bandari hiyo ikiwa ni moja ya “masharti ya ajabu.”

Amesema Serikali inaendeleza ujenzi wa Bandari ya Tanga ili kuhudumia bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga lakini wawekezaji hao hawataki uendelezaji wa bandari wa namna hiyo.

“Ni nchi gani hiyo ambayo unajenga Bandari ya Da res Salaam, tunachimba sasa hivi bath (gati) 0 hadi 10 kwa gharama ya Sh1.2 trilioni, tumekopa fedha… na contractor (mkandarasi) yupo na inawezekana at the end of this year (mwishoni mwa mwaka) watamaliza…tutakuwa tunapata mizigo karibu ya mara tatu inayoingia..leo hii unakwenda kudump (kutupa) hela pale Bagamoyo maana yake siutakuwa unaua bandari hii iliyoachwa na Nyerere?” amehoji Rais Magufuli.