October 7, 2024

Majaliwa asisitiza matendo mema sikukuu ya Eid

Amewataka waislamu wote nchini kutenda matendo mema pamoja na kuwakumbuka yatima na wajane.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa swala ya Eid El Fitr katika msikiti wa Anwar uliopo Msasani jijini Dar es Salaam. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Amewataka waislamu wote nchini kutenda matendo mema pamoja na kuwakumbuka yatima na wajane.
  • Waumini wa dini zote pia wametakiwa kuendelea kuwa wamoja, kuimarisha mshikamano na kuvumiliana.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka waislamu wote nchini watumie sikukuu ya Eid el Fitr kwa kutenda matendo mema pamoja na kuwakumbuka yatima na wajane.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Juni 5, 2019) wakati wa swala ya Eid El Fitr katika msikiti wa Anwar uliopo Msasani jijini Dar es Salaam.

“Leo ni siku kubwa na muhimu waislamu wanahitimisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kusherehekea siku kuu ya Eid El Fitr, hivyo tuendeleze matendo mema,” amesema Majaliwa. 

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu inaeleza kuwa wakati huu ni mzuri kwa kuimarisha mshikamano miongoni mwa waumini wa Kiislamu na madhehebu mengine na kuhakikisha wanayaendeleza mambo mema yote waliyoamriwa katika dini yao.

“Tumeona utulivu uliojitokeza katika mwezi mtukufu, na jambo hili limesisitizwa na viongozi wa dini. Tuendelee kuwa wamoja, tuimarishe mshikamano na tuvumiliane,” amesisitiza Majaliwa.


Zinazohusiana:


Pia, Waziri Mkuu amewakumbusha wazazi na walezi kuwaongoza watoto kwa kuwapa mafundisho ya dini yatakayowawezesha kumjua Mwenyezi Mungu na kuwa raia wema.

Kwa upande wake, Imamu wa msikiti huo, Sheikh Mhina amesema waislamu wanatakiwa kuitumia siku ya leo kwa kuhamasisha amani pamoja na kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo.

Pia amewasisitiza wayaendeleze mema yote waliyoyafanya katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kuwaheshimu na kuwajali wazazi wao.