Tanzania kuinadi kahawa yake katika maonyesho ya kimataifa
Ubalozi wa Tanzania nchini China umeeleza kuwa unatumia fursa ya Maonyesho ya Kimataifa ya Utamaduni 2019 ya Beijing, China kuongeza wigo wa masoko kimataifa kwa kuwatanisha wafanyabiashara wa Tanzania na makampuni ya China yanayonunua kahawa.
- Utatumia fursa hiyo kuongeza wigo wa masoko wa kahawa ya Tanzania inayouzwa kimataifa.
- Wageni watakaotembelea banda la Tanzania wataona na kuonja aina mbalimbali za kahawa ya Tanzania.
- Wafanyabiashara wa Tanzania kukutanishwa na makampuni ya China yanayonunua kahawa.
Dar es Salaam. Ubalozi wa Tanzania nchini China umeeleza kuwa unashiriki katika Maonyesho ya Kimataifa ya Utamaduni 2019 ya Beijing, China na utatumia fursa hiyo kuinadi kahawa inayozalishwa nchini ili kuongeza wigo masoko kimataifa.
Maonyesho hayo ambayo yanatambulika kama “International Horticultural Exhibition 2019 yalizinduliwa Aprili 29, 2019 na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 7 mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Tanzania nchini China, inaeleza kuwa Juni 25, 2019 itakuwa ni siku ya Tanzania katika maonyesho hayo ambapo pamoja na shughuli nyingine katika banda la Tanzania itaitumia siku hiyo kuinadi kahawa ya Tanzania kwa wageni watakaotembelea.
Wageni watapata fursa ya kuona na kuonja aina mbalimbali za kahawa ya Tanzania zitakazokuwepo katika maonyesho hayo.
Tarehe 25 Juni 2019 ni siku ya Tanzania katika maonesho ya kimataifa ya Horticulture yanayoendelea Beijing. Moja ya matukio yatakayofanyika siku hiyo ni “Tanzania Coffee Cupping (tester)” ambapo wageni watapata fursa ya kuona na kuonja aina mbalimbali za kahawa kutoka Tanzania pic.twitter.com/UhMpyXYIIK
— Tanzania Embassy in China (@TZEmbassy) June 1, 2019
Kutokana na umuhimu wa siku hiyo, ubalozi unawakaribisha wadau wa kahawa nchini kushiriki katika hafla ya kuonja kahawa (Tanzania Coffee Cupping (tester) ambapo watapata fursa ya kukutana na makampuni ya China yanayonunua kahawa.
“Vilevile watapata nafasi ya maalum ya kuonyesha bidhaa zao katika banda la maonyesho la kahawa wiki nzima,” inaeleza taarifa hiyo iliyowekwa katika ukurasa wa Twitter wa ubalozi wa Tanzania nchini China.
Soma zaidi:
- Uzalishaji kahawa kuimarika msimu 2019/2020
- Mnada wa kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Uzalishaji wa kahawa kushuka msimu ujao
Kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Sekta ya Kahawa Tanzania iliyotolewa Aprili 2019 na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), watumiaji wakubwa wa kahawa ya Tanzania ni pamoja na Japani kwa asilimia 27, Ujerumani (17%), Ubelgiji (12%) na Italia (10%) huku masoko mpya ambayo yameanza kufikiwa ni pamoja na India, Urusi, Afrika Kusini, Australia na China.