November 24, 2024

Uswisi kuwekeza Sh55 bilioni katika sekta ya ufundi stadi Tanzania

Fedha hizo zitatumika katika programu ya Stadi za Ajira (SET) ili kuwapatia vijana ujuzi na stadi za kazi kuwawezesha kujiajiri na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.

  • Fedha hizo zitatumika katika  programu ya Stadi za Ajira (SET)  ili kuwapatia vijana ujuzi na stadi za kazi kuwawezesha kujiajiri na kuchangia katika ukuaji wa uchumi. 
  • Watakaofaidika na programu hiyo ni vijana kati ya miaka 15 na 24 hasa wasichana.
  • Itasaidia kupunguza umaskini kwa vijana na kuwawezesha kujiajiri na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.

Dar es Salaam. Uswisi  inakusudia kutoa Sh55 bilioni kwa Tanzania kwa ajili ya programu ya maendeleo ya ufundi stadi inayolenga kuwapatia vijana ujuzi na stadi za maisha zitakazowasaidia kujiajiri katika kilimo na kilimo biashara ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Fedha hizo zitatolewa kupitia programu ya Stadi za Ajira Tanzania (SET) ambayo itatekelezwa na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC) katika kipindi cha miaka 12 ili kuboresha mafunzo ya ufundi stadi nchini Tanzania. 

Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Florence Mattli ameeleza leo (Mei 31, 2019), wakati wa uzinduzi wa awamu ya kwanza ya programu hiyo, kuwa fedha hizo zitasaidia kuwaondolea vijana umaskini na kuboresha maisha yao kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi ili kujiajiri katika sekta mbalimbali. 

“Maendeleo ya ufundi stadi yanalenga zaidi katika kuwapa vijana ujuzi na stadi zinazohitajika kuwawezesha kushindana katika soko la ajira,” amesema Balozi Mattli. 

Amesema mgao wa fedha hizo, pia utasaidia kuzijengea uwezo taasisi zinazotoa mafunzo ya ufundi stadi ikiwemo VETA kwa kuboresha miundombinu na ujuzi wanaoutoa ili kuwafikia vijana wa kada zote hasa waishio vijijini. 

“Katika mkoa wa Morogoro, SET itafanya kazi na Chuo cha Ualimu cha Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) kuongeza ujuzi wa walimu na kuendeleza mbinu bunifu za ufundishaji hasa njia za kidijitali,” amesema. 

Kulingana na ripoti ya Shirika la Kazi Dunia (ILO), asilimia 82 ya vijana wa Tanzania hujikuta katika ajira hatarishi zisizo rasmi, zisizo hitaji ujuzi mkubwa na zisizo na thamani katika kuboresha maisha yao. 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Florence Mattli wakizindua rasmi programu ya Stadi za Ajira Tanzania (SET) leo jijini Dar es Salaam. Picha|Daniel Samson.

Mtaalam wa uchumi, Profesa Samuel Wangwe amesema taasisi za ufundi stadi zina mchango mkubwa katika maendeleo na viwanda hasa katika kuwaandaa vijana wenye ujuzi na weledi wa kiufundi. 

Amesema ili kuwa na uwiano mzuri wa ajira na Taifa kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025, vyuo hivyo vinapaswa kuongezewa nguvu ya kuwafikia vijana wengi hasa waishio vijijini ambao wamezungukwa na fursa nyingi zinazohitaji ujuzi na  teknolojia rahisi kuziibua na kuzitumia kwa manufaa yao. 

SET inalenga vijana kati ya miaka 15 na 24, hasa wale ambao hawafikiwi na mfumo rasmi wa mafunzo ya ufundi stadi ikiwa ni pamoja na wasichana.

Programu hiyo itafanya kazi kwa karibu na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Taasisi ya Sekta Binafsi ya Tanzania (TPSF) na asasi za kiraia ili kufungua fursa zaidi katika kilimo na kilimo biashara. Vijana wapatao 16,000 hasa wasichana wanatarajiwa kufaidika na programu hiyo.


Soma zaidi: Toolboksi: Teknolojia inayowaunganisha vijana na fursa za ufundi stadi Tanzania


Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Joyce Ndalichako ameihakikishia Uswisi kuwa fedha hizo zitatumika vizuri na kuwafikia vijana ili kuongeza nguvu kazi itakayotumika katika shughuli za kiuchumi nchini. 

Amesema Serikali inaendelea na uboreshaji wa vyuo vya ufundi stadi ikiwemo kujenga vipya ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa na wanaopata ujuzi na stadi za maisha. 

SET pia inatekelezwa sambamba na Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Stadi za Ufundi (NSDS 2016-2026) ambao unalenga kukuza fursa  za maendeleo ya stadi zinazotokana na mahitaji ya ajira.