October 6, 2024

Maumivu kwa makampuni matano soko la hisa Dar

Thamani ya hisa za kampuni hizo ikiwemo benki ya KCB zimeshuka kwa viwango tofauti.

Kampuni ya Vodocom ndiyo iliyofanya vizuri zaidi leo baada ya kampuni hiyo kuongoza kwa kuuza kiwango kikubwa cha hisa. Picha|Mtandao. 


  • Thamani ya hisa za kampuni hizo ikiwemo benki ya KCB zimeshuka kwa viwango tofauti. 
  • Vodacom yatawala soko la hisa baada ya kuuza kiwango kikubwa zaidi cha hisa.
  • Hakuna hata kampuni moja ambayo thamani ya hisa zake imepanda.

Dar es Salaam. Wawekezaji wa kampuni matano katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ikiwemo benki ya KCB leo watalala na maumivu baada ya thamani ya hisa za kampuni hizo kushuka kwa viwango tofauti ikilinganishwa na jana Mei 28, 2019.

Ripoti ya soko ya siku ya DSE ya Mei 29 inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa jioni ya leo kampuni ya uwekezaji ya NICO ndiyo iliyofanya vibaya zaidi baada ya thamani ya hisa zake kushuka kwa asilimia 2.86 ambapo wawekezaji wake wamepoteza Sh5 kwa kila hisa moja. 

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa  thamani ya hisa moja ya NICO ilikuwa ni Sh170 kutoka Sh175 iliyorekodiwa jana.

Kampuni nyingine ambazo thamani ya hisa zake zimeshuka ni pamoja na benki ya KCB ambayo imeporomoka kwa asilimia 1.09, kampuni ya habari ya NMG (asilimia 0.83), kampuni ya bia ya Afrika Mashariki-EABL (asilimia 0.43) na JHL (asilimia 0.22).


Zinazohusiana: 


Wakati wawekezaji wa kampuni hizo wakiugulia maumivu, hakuna hata kampuni moja ambayo thamani ya hisa zake imepanda katika soko hilo huku nyingi zikibaki katika viwango vilivyokuwepo jana zikiwemo Vodacom, na benki ya CRDB, DCB na Acacia. 

Hata hivyo, kampuni ya Vodocom ndiyo iliyofanya vizuri zaidi leo baada ya kampuni hiyo kuongoza kwa kuuza kiwango kikubwa cha hisa. 

Vodacom imeuza hisa 2.4 milioni sawa na asilimia 99.5 ya hisa zote zilizouzwa sokoni leo huku ikifuatiwa kwa mbali na NICO ambayo imeuza hisa 10,000 na kampuni ya saruji ya TPCC (111).