November 24, 2024

New York kutunga sheria ya kuzuia watembea kwa miguu kutumia simu barabarani

Sheria hiyo inapendekeza kuwa watu wasiruhusiwe kuandika meseji, kuangalia barua pepe na kuperuzi mtandaoni, isipokuwa kwa dharura wanapokatiza mitaa ya jiji hilo.

Ukuaji  wa matumizi ya simu janja, unaweza kuwa na mchango mkubwa wa vifo vya watembea kwa miguu. Picha| Mtandao.


  • Sheria hiyo inapendekeza kuwa watu wasiruhusiwe kuandika meseji, kuangalia barua pepe na kuperuzi mtandaoni, isipokuwa kwa dharura wanapokatiza mitaa ya jiji hilo. 
  • Hatua hiyo itasaidia kupunguza ajali za watembea kwa miguu.
  • Baadhi ya wadau wamepinga sheria hiyo wakidai haina manufaa. 

Huenda siku zijazo itakuwa ni kinyume na sheria kwa watembea kwa miguu katika jiji la New York nchini Marekani kutumia simu za mkononi wakati wakikatiza barabara za mitaa ya jiji hilo, ikiwa ni hatua kupunguza ajali za barabarani.

Hatua hiyo inakuja baada ya Senata John Liu kutoa hoja ya kushinikiza bunge la seneti la New York kujadili na kupitisha muswada wa sheria ya kuzuia matumizi ya vifaa vya elektroniki barabarani. 

Sheria hiyo inapendekeza kuwa watu wasiruhusiwe kuandika meseji, kuangalia barua pepe na kuperuzi mtandaoni, isipokuwa kwa dharura. 

Ikiwa mtu yeyote atakakaidi sheria hiyo atozwe faini ya dola za Marekani 25 hadi 250 (Sh57,448 hadi Sh574,480).

Muswada huo ulifikishwa katika bunge hilo kwa mara ya kwanza mwaka jana na Mbunge Felix Ortiz lakini ulikuwa bado hujajadiliwa mpaka ulipoibuliwa tena na Seneta Liu.

“Ni vigumu kutambua idadi ya watu wanaotuma ujumbe wakati wa kutembea, lakini inasikitisha sana kuona watu wanaendelea kuandika meseji wakati wa kuvuka barabara,” amesema Liu alipohojiwa na shirika la habari la CNN. 

Ili muswada huo ukubaliwe lazima uidhinishwe na kamati ya usafiri katika mabunge yote mawili (Bunge la Wawakilishi na Seneti) kabla ya kabla ya kupigiwa kura na kuwa sheria.


Zinazohusiana: 


Mwenyekiti wa kamati ya usafiri wa bunge la Senati, Sen Kennedy, tayari ameonyesha mashaka juu ya muswada huo.

“Sikubaliani na dhana hiyo kwa  sasa,” Kennedy amesema katika taarifa kwa CNN. “Kama mtu ambaye nimejitolea katika mageuzi makubwa ya usalama wa watembea kwa miguu kwa miaka yote, ninaona kipaumbele kiwe ulinzi na usalama kwa watu wote wa New York.”

Ripoti ya Chama cha Magavana wa Usalama barabarani ya mwaka 2019 inaonyesha kuwa mwaka 2018 watembea kwa miguu 6,227 walifariki dunia katika ajali za barabarani nchini Marekani. 

Hata hivyo, ripoti hiyo inabainisha kuwa ukuaji  wa matumizi ya simu janja, unaweza kuwa na mchango mkubwa wa vifo vya watembea kwa miguu.