October 7, 2024

Vituo vipya saba vya madini kuanzishwa 2019-2020

Serikali imesema mpaka sasa kuna vituo 21 na inatarajia kuongeza vingine saba ili kurahisisha biashara ya madini katika maeneo ya machimbo.

Dhahabu ni miongoni mwa madini yanayopatikana Tanzani lakiniwachimbaji wadogo wanatafuta namna ya kufaidika nayo. Picha|Mtandao.


  • Serikali imesema mpaka sasa kuna vituo 21 na inatarajia kuongeza vingine saba ili kurahisisha biashara ya madini katika maeneo ya machimbo.
  • Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli la kujenga vituo hivyo katika maeneo ya migodi. 

Dar es Salaam. Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 wanatarajia kufungua masoko saba mapya ya ununuzi wa madini ili kurahisisha biashara hiyo na kuwanufaisha wafanyabiashara wadogo wadogo. 

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Januari 09, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati ambapo alimuagiza Biteko kusimamia uanzishwaji wa vituo vya ununuzi wa madini katika maeneo yenye migodi ukiwemo mji wa Geita. 

Biteko aliyekuwa akizungumza na Idara ya Habari Maelezo mwishoni mwa wiki, amesema mpaka sasa kuna maduka 21 yanatumika kama vituo vya ununuzi wa madini kote nchini. 

Baadhi ya mikoa ambayo imeshafungua masoko ya kuuza madini ni pamoja na Geita, Dodoma, Mwanza, Tabora, Shinyanga, Morogoro na Mbeya. 

Amesema katika mwaka wa fedha 2019/2020 masoko mengine saba yanatarajiwa kufunguliwa katika maeneo mbalimbali nchini ili kutekeleza agizo la Rais Magufuli la kuwa na vituo hivyo katika maeneo ya migodi. 


Zinazohusiana:


Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana baada ya kufunguliwa kwa maduka 21 ya ununuzi wa madini, amesema kilo 409.3 za dhahabu yenye thamani ya Sh34.3 bilioni imeuzwa katika kipindi cha mwezi mmoja kutoka Machi, 17 hadi Aprili, 17, 2019. 

“Katika kilo hizo, mkoa wa Geita umeongoza kwa kufanya biashara ya  jumla ya kilo 289, Kahama kilo 44, Mara kilo 13, lakini cha kufurahisha zaidi ni  kwa Wilaya ya Chunya ambako jumla ya kilo 52 zimeuzwa katika soko hilo zikiwa ni siku chache toka kufunguliwa kwake,” amesema Biteko.

Licha ya mafanikio hayo yaliyofikiwa katika kipindi kifupi, Serikali imesema inashughulikia changamoto ndogo ndogo ikiwemo upatikanaji wa wafanyakazi, mashine za XRF (Mashine za kupima ubora wa madini) katika vituo hivyo na idadi ya watoa vibali katika maeneo ya machimbo.

Pia amewataka wachimbaji wadogo na madalali wa madini kuhakikisha kuwa wanatumia masoko hayo kikamilifu  na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni.