October 7, 2024

Mwakyembe azipa somo taasisi za mawasiliano Afrika

Amezitaka zijitofautishe na vyombo vya habari vya nje vya bara hilo ambavyo amedai vimekuwa vikiripoti zaidi mambo mabaya

Amesema ni wajibu wa vyombo  vya habari kutumia majukwaa yao kutetea na kutangaza mafanikio yaliyopo Afrika. Picha|Mtandao.


  • Amezitaka zitoe kipaumbele katika kutangaza zaidi maendeleo ya bara hilo.
  • Amezitaka zijitofautishe na vyombo vya habari vya nje vya bara hilo ambavyo amedai vimekuwa vikiripoti zaidi mambo mabaya. 
  • Awakumbusha vijana kufuatilia historia ya Afrika na kuweka mikakati thabiti ya kujikwamua kiuchumi.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema taasisi za habari na mawasiliano barani Afrika zina wajibu kulitangaza bara hilo kwa mambo mema yanayofanyika na “kuachana na propaganda za magharibi”. 

 Dk Mwakyembe aliyekuwa akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mawasiliano Barani Afrika jijini Dar es Salaam, amesema taasisi hizo hazina budi kuonyesha uthubutu kwa kuweka sera zinazoakisi maendeleo na kuyatangaza kwa wananchi na nje ya bara hilo.

Akizungumzia vyombo vya habari vya Afrika,  amevitaka kujitofautisha na vyombo vya nje ya bara hilo ambavyo amedai vimekuwa vikipotosha na kubeza kwa makusudi mambo mazuri yanayotekelezwa na yaliyotekelezwa na nchi za Afrika.

Amebainisha kuwa maudhui ya vyombo vya habari vilivyopo nje ya bara la Afrika vinavyoongozwa na mataifa makubwa huripoti na kutangaza zaidi mambo mabaya yanayohusu Afrika ikiwemo njaa, magonjwa, vurugu za kisiasa na vita. 


Zinazohusiana:


Amesema ni wajibu wa vyombo  vya habari kutumia majukwaa yao kutetea na kutangaza mafanikio yaliyopo Afrika.

“Wakati Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Kenneth Kaunda wa Zambia walipoamua kujenga reli ya Tazara, walipingwa vikali sana na wakoloni waliotutawala na wengine waliita reli ile kuwa ni bamboo (mianzi) lakini ni taifa moja tu la China walitusaidia na leo hii reli ile ndiyo ndefu zaidi katika bara la Afrika yenye urefu wa kilometa 1,860,” amesema Dk Mwakyembe.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amewataka vijana wa Afrika ikiwemo Tanzania kujifunza historia ya bara lao ili kuweza kufahamu wapi walipotoka na wapi wanapoelekea badala ya kulalamika pasipo kuweka mikakati ya namna bora ya kupiga hatua za kujiletea maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.

Naye Rais wa Chama cha Maafisa Uhusiano wa Sekta Tanzania (PRST), Loth Makuza amesema kuwa taasisi yake kwa kutumia Tehama imeweza kutengeneza majukwaa yanayotangaza masuala mbalimbali ya kimaendeleo yaliyofikiwa katika nchi za Afrika, lengo likiwa ni kubadili mtazamo hasi wa bara la Afrika katika diplomasia ya kimataifa hasa katika nyanja za kiuchumi na kijamii.