Serikali kutolea uamuzi bei mpya za maji zilizopangwa kupaa kwa asilimia 80
Imesema inapitia viwango vipya vya bili za maji vilivyopendekezwa na Ewura kabla ya kuanza kutumika.
Maji ni uhai kwa binadamu. Huduma hiyo inatakiwa kuwafikia watu wote kwa gharama wanazoweza kuzimudu. Picha|Mtandao.
- Imesema inapitia viwango vipya vya bili za maji vilivyopendekezwa na Ewura kabla ya kuanza kutumika.
- Viwango hivyo vimepanda kwa asilimia 80 kutoka bei ya sasa.
- Mbunge Pauline Gekul adai wananchi hawawezi kumudu bei mpya.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itapitia viwango vipya vya bili za maji vilivyopendekezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ili kuona kama Watanzania wanaweza kumudu kulipa gharama hizo za maji katika maeneo yao.
Inaelezwa kuwa Ewura inapendekeza viwango vya bili za maji kupanda kwa asilimia 80 kutoka bei ya sasa inayolipwa na wateja wanaopata huduma hiyo muhimu kutoka kwa mamlaka za maji nchini.
Majaliwa ametoa msimamo huo wa Serikali bungeni leo (Mei 23, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul aliyetaka kufahamu Serikali inatoa kauli gani juu ya ongezeko hilo la zaidi ya asilimia 80 ya ankara za maji nchini wakati wananchi waliomba bili hizo zisipande.
Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema azma ya Serikali ni njema na kwa kila huduma inazotoa kwa wananchi inaangalia uwezo wao wa kifedha wa kumudu huduma husika.
Amesema watapitia viwango hivyo baada ya Ewura kuwasilisha mapendekezo yao serikalini kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho wa bei itakayotumika nchini kote.
“Nimepata taarifa kwamba Ewura, Wizara ya Maji kupitia wakala wamekaa vikao vyao wameshatoa taarifa ya mwisho ya gharama imefikia kwa kiwango ulichokitaja imepanda kwa asilimia 80.
“Kwa hiyo ni jukumu la Serikali baada ya kuwa imepata matokeo yale, baada ya mjadala wao wataleta serikalini tuone kama viwango walivyotoa vinawezesha Watanzania kupata huduma hiyo? Na tunapogundua hawawezeshwi kupata huduma hiyo basi Serikali itafanya maamuzi mengine dhidi ya hilo,” amesema Majaliwa.
Zinazohusiana:
- Tanzania kuendelea kutoa ushirikiano utunzaji bonde la mto Nile
- Visima kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama nchini?
Amebainisha kuwa amepata taarifa kuwa hata wadau hawakuweza kupata fursa ya kusikilizwa wakati wa kupitisha viwango hivyo lakini Serikali inalifanyia kazi suala hilo.
Awali wakati akiuliza swali lake, Gekul amesema anafahamu mchakato wa Serikali kupandisha bili za maji kupitia mamlaka za maji na kufanya public hearing (maoni ya umma) na mwisho Ewura waweze kufanya maamuzi ya bili hizo.
“Ewura wamemaliza mchakato, bahati mbaya sana maoni ya wananchi hayajazingatiwa, bili hizi za maji kote nchini zimepanda kwa asilimia 80. Mfano mtumiaji wa maji nyumbani alikuwa analipa uniti moja kwa Sh1,195 imepanda kuanzia hapo mpaka 1,800,” amesema Gekul.