November 24, 2024

Unataka kupumzika? Hifadhi ya Taifa ya Arusha ni mahali sahihi

Hifadhi hiyo iko umbali wa kilomita 62 kutoka katika mji wa kitalii wa Arusha na inasifika kwa vivutio mbalimbali ikiwemo Mlima Meru, Ziwa Momella na bonde la Ngurdoto.

  • Hifadhi hiyo iko umbali wa kilomita 62 kutoka katika mji wa kitalii wa Arusha.
  • Imesheheni vivutio mbalimbali lakini zaidi ni maarufu kwa mbega weusi na weupe.
  • Mlima Meru, Ziwa Momella na bonde la Ngurdoto ni fahari ya hifadhi hiyo. 

Dar es Salaam. Ni mwendo wa saa moja kukamilisha safari ya kilomita 62 kutoka mji wa kitalii wa Arusha hadi kuifikia hifadhi ya Taifa ya Arusha iliyopo kaskazini mwa Tanzania. 

Hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 328.4 inasifika zaidi kwa upatikanaji wa wanyama jamii ya tumbili wajulikanao kama mbega weusi na weupe ambao huipamba mandhari nzuri ya hifadhi hiyo. 

Tofauti na hifadhi nyingine zilizopo Tanzania, hifadhi ya Taifa ya Arusha kwa mujibu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), ina maeneo makuu matatu muhimu kwa kuvutia watalii wengi ambayo ni  bonde la Ngurdoto (Ngurdoto Crater), maziwa ya Momella ambayo kila moja hutoa mandhari tofauti pamoja na mlima Meru wenye urefu wa mita 4,566 sawa na futi 14,990, hali inayoifanya hifadhi hiyo kuwa na mazingira ya baridi. 

Licha ya umaarufu wake wa kuwa na tumbili, watalii wanaotaka kutembelea hifadhi hiyo watajionea wanyama wengine kama twiga, pundamilia, nyati, tembo na digidigi. 

Pia unaweza kuwaona chui wakibarizi katika vivuli vya matawi ya miti inayokingwa na maanguko ya maji huku makundi kadhaa ya batamaji yakitafuta wadudu katika maziwa ya Momella. 

Mlima Meru ni fahari ya hifadhi ya Taifa ya Arusha. Picha|Mtandao.

TTB inaeleza kuwa zaidi ya hapo ni kupatikana kwa aina 400 za ndege ndani ya hifadhi hiyo ambao huipamba misitu ya asili ya Ngurdoto na maporomoko ya maji ya Tululusia na Maio ndiyo marefu zaidi ndani ya hifadhi.

Maporomoko ya Tululusia yana urefu wa takribani mita 28 na yapo karibu na lango la Momella, wakati yale ya Maio yapo pembezoni mwa barabara iendayo mlimani.


Zinazohusiana:


Shughuli za utalii ndani ya hifadhi

Shughuli za utalii katika hifadhi hiyo ambayo ni miongoni mwa hifadhi sita zilizopo kaskazini mwa Tanzania zinahusisha kupanda mlima hadi kilele cha Mlima Meru au kufika moja wapo ya mabanda ya watalii; matembezi ya miguu ambayo huchukua hadi saa manne; utalii wa kutembea kwa magari; utalii wa kuendesha mitumbwi katika ziwa dogo la Momella; na utalii wa kupanda farasi ambao huratibiwa na kampuni za utalii zilizopewa leseni ya kutoa huduma ndani ya hifadhi. 

Kwa upande wake, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) inaeleza kuwa wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hiyo ni kati ya mwezi Juni na Februari ingawa mvua inaweza kunyesha mwezi Novemba.

Ndani ya hifadhi kunapatikana huduma za malazi zenye hadhi tofauti  kama hoteli, nyumba za wageni na makambi ya kupiga mahema lakini wageni wanaweza kupata malazi nje ya hifadhi katika miji midogo ya Usa River and Arusha Mjini. 

Kwako wewe unayejipanga kupata mapumziko ya katikati ya mwaka, basi hifadhi ya Taifa ya Arusha ni sehemu salama kwasababu utakutana na mandhari nzuri ya utulivu katika kipindi chote utakachokuwepo katika hifadhi hiyo.

Watalii wanaotembelea hifadhi ya Taifa ya Arusha wanapata fursa ya kufanya matembezi ya farasi katika maeneo mbalimbali hifadhini. Picha|Mtandao.