October 6, 2024

Maeneo matano ya kimkakati kuboresha kilimo 2019-2020

Maeneo hayo ni pamoja na uanzishwaji wa bima ya mazao, upitiaji wa mfumo wa upatikanaji pembejeo za kilimo na usajili wa wakulima

  • Maeneo hayo ni uanzishwaji wa bima ya mazao, upitiaji wa mfumo wa upatikanaji pembejeo za kilimo na usajili wa wakulima
  • Eneo nyingine ni kuipitia Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 na sheria mbalimbali zinazosimamia kilimo. 
  • Lakini wizara itakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha mikakati hiyo inatekelezwa kwa wakati kama ilivyopangwa.

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameainisha maeneo matano ya kimkakati ambayo wizara yake itayafanyia maboresho katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 ikiwemo kuanzisha bima ya mazao ili kuimarisha usimamizi wa sekta kilimo na kuwapatia wakulima huduma kwa urahisi zaidi.

Akizungumza bungeni jana (Mei 17, 2019) wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka unaofuata, Hasunga amesema licha kuwa na vipaumbele vingi na mikakati mbalimbali, kama wizara wanaona yapo maeneo muhimu ambayo yakitekelezwa kwa wakati yataleta matokeo makubwa katika sekta ya kilimo. Maeneo hayo ni pamoja na:

Mapitio ya sera na sheria 

Wizara hiyo imeanza na itaendelea kuipitia Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013 na sheria mbalimbali kwa lengo la kubaini maeneo ambayo yatapaswa kuhuishwa ili kwenda na hali halisi ya sasa na mwelekeo wa Serikali wa kubadili kilimo cha Tanzania kuwa kilimo cha kibiashara.  

“Mtazamo wa Wizara ni kuwa na Sheria moja itakayosimamia rasilimaliwatu, matumizi bora ya pembejeo, ardhi ya kilimo na maeneo mengine muhimu,” amesema Hasunga.

Sera na sheria nzuri zinazotekelezeka ni muhimu katika ukuaji wa sekta ya kilimo nchini. Picha|Mtandao.

Mifumo ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo

Eneo nyingine ni kupitia mifumo ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo ambapo tayari wizara imeanza zoezi la kupitia kwa kina mifumo iliyopo ya uzalishaji, uagizaji na usambazaji wa mbegu, mbolea na viuatilifu. 

Hasunga amesema mifumo iliyopo sasa inatofautiana kwani kuna baadhi ya Bodi za Mazao zinazojihusisha na uagizaji  na usambazaji wa pembejeo na wakati mwingine vyama vya ushirika vinaagiza na kusambaza pembejeo kwa wanachama wao.

Mkanganyiko mwingine ni wakulima kununua pembejeo moja kwa moja kutoka kwa wafanyabiashara na pia mbolea kwa sasa inaagizwa kwa mfumo wa pamoja (Bulk Procurement). 

“Malengo yetu ni kukamilisha mapitio hayo na kupata majawabu ya mfumo bora ifikapo Juni 2019, ili mwaka 2019/2020 tuwe na mfumo madhubuti utakaokuwa na tija kwetu sote,” amesema Hasunga.


Zinazohusiana: 


Kuimarisha utafutaji wa masoko ya mazao ya kilimo

Katika mwaka 2019/2020, Wizara ya Kilimo imesema itakiimarisha kitengo cha masoko kwa kukijengea uwezo wa kufanya uchambuzi na utafutaji wa masoko ndani na nje ya nchi.

“Aidha, elimu itaendelea kutolewa kwa wakulima ili wazalishe kulingana na mahitaji ya soko. Vilevile, tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na taasisi nyingine zinazohusika na masoko nchini ikiwemo TANTRADE (Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania) na Soko la Bidhaa (TMX),” amebainisha Hasunga katika hotuba yake.

Usajili wa wakulima

Katika hatua nyingine wizara hiyo yenye jukumu la kusimamia na kuendeleza shughuli za kilimo imeeleza kuwa itaimarisha kanzidata (Database) ya wakulima na kuendelea na usajili wa wakulima wa mazao mchanganyiko kwa kushirikiana kwa karibu na vyama vya ushirika na taasisi za wakulima kama vile Tanganyika Farmers Association (TFA). 

Hata hivyo, Hasunga amewaomba Wabunge wamsaidie kuhamasisha wakulima katika maeneo yao ili watakapofikiwa na zoezi la uandikishaji watoe ushirikiano na waelewe kwamba zoezi hilo ni la kuwasaidia kupata huduma bora za Kilimo.

Pia hajaweka wazi vigezo vinavyohitajika kwa mkulima kusajiliwa na jinsi watakavyowafikia wakulima wote ili kuhakikisha wanatambuliwa rasmi na mamlaka husika. 

Usajili wa wakulima katika regista utasaidia kuwa na takwimu sahihi za idadi yao jambo litakalosaidia katika kufanya maamuzi sahihi katika sekta ya kilimo. Picha|Mtandao.

Uanzishwaji wa bima ya mazao

Katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2019/2020 imeanza kujadiliwa na Wabunge kabla ya kuidhinishwa, Hasunga ameweka wazi nia ya Serikali ya kuanzisha Bima ya Mazao ili kumwezesha mkulima kulipwa fidia pale anapopata hasara. 

Amesema maandalizi yanaendelea kufanyika “ili katika mwaka 2019/2020 tuwe angalau na aina mbili za mifumo ya Bima ya mazao inayoweza kutumika hapa nchini.” 

Hata hivyo, katika utekelezaji wa mkakati huo, wizara itakuwa na kibarua kigumu cha kutafuta takwimu sahihi za wakulima, hali ya hewa pamoja na uzingatiaji wa kanuni bora za Kilimo.