November 24, 2024

Hizi ndizo sababu kwanini hoteli zinatumia mashuka meupe

Ni sehemu ya hoteli kujihakikishia viwango vya usafi vinavyopendekezwa katika maeneo yao na kubaini uchafu kwa haraka ikiwemo madoa na mawaa.

  • Hutumika kubaini uchafu kwa haraka ikiwemo madoa na mawaa.
  • Rangi nyeupe ni ishara ya ufahari na mvuto kwa wageni wanaopenda sehemu nadhifu.
  • Ni sehemu ya hoteli kujihakikishia viwango vya usafi vinavyopendekezwa katika maeneo yao. 

Kama wewe ni msafiri ambaye amekuwa akitumia hoteli au nyumba za kulala wageni katika maeneo tofauti uliyotembelea, basi utakuwa umegundua kitu tofauti katika vyumba vya hoteli ambavyo umewahi kulala.

Kitu hicho ni mashuka meupe yanayotumika kitandani. Hili limekuwa likifanyika karibu katika hoteli zote duniani. Lakini umewahi kujiuliza sababu za kwanini wanatumia mashuka au mablanketi meupe ya kujifunika wakati umelala?

Sababu kubwa ni kuwarahishia wahudumu kubaini madoa, mawaa au uchafu wakati wakifua mashuka hayo ikizingatiwa kuwa yanatumika na watu wengi, hivyo yanatakiwa yawe safi wakati wote ili kulinda afya za watumiaji. 

Kama yangekuwa na rangi nyingine ingekuwa ni vigumu kubaini uchafu ambao unasababishwa na wageni wakati wakitumia. 


Soma zaidi:


Mashuka meupe ni njia mojawapo ya wamiliki wa hoteli kujihakikishia kwamba wanazingatia viwango vya usafi. Kama ilivyo kwa matajiri wanaopendelea kuvaa nguo nyeupe kudhihirisha kuwa wanaweza kujiweka katika hali ya usafi wakati wote, basi hali hiyo ni zaidi sana kwa hoteli zinazopokea wageni wa kila aina kuweka mazingira yao safi ikiwemo vitandaa na vifaa vyake. 

Sababu kubwa ni kuwarahishia wahudumu kubaini madoa, mawaa au uchafu wakati wakifua mashuka hayo ikizingatiwa kuwa yanatumika na watu wengi, hivyo yanatakiwa yawe safi wakati wote ili kulinda afya za watumiaji. Picha|Mtandao.

Lakini wachambuzi wa masuala ya biashara wanasema rangi nyeupe inadhihirisha ishara ya ufahari na anasa. Kwa mtu kulala sehemu anayohisi ni fahari inamvutia na kumpatia usingizi mnono na mwanana. 

“Mtazamo na wazo la kitanda cheupe ni muhimu,” anasema Erin Hoover, Makamu wa Rais wa Ubunifu katika hoteli za Westin na Sheraton wakati akihojiwa na mtandao wa HuffPost na kuongeza kuwa, “Kitu chochote kuhusu kitanda cheupe kinaonyesha ufahari na usingizi mzuri wa usiku.”

Rangi nyeupe sio tu inatumika kitandani, lakini muonekano na vifaa vya vyumba vya hoteli nyingi vina rangi hiyo. Mathalani, mataulo, vitambaa, karatasi nyepesi za kukaushia mikono huwa katika rangi nyeupe. 

Hiyo pia huwarahisishia wahudumu kufua mashuka na nguo zingine kwa pamoja bila kuzitenganisha kutokana na rangi zake.

Kwako rangi nyeupe katika nyumba yako au mavazi unayovaa inamaanisha nini? Inakupa raha kama wanayopata wageni wanaotumia hoteli mbalimbali duniani?