Tanzania yatajwa nchi zinazotegemea kuuza bidhaa ghafi duniani
Tanzania inategemea zaidi kusafirisha madini na vito vya thamani ili kujipatia mapato lakini hali hiyo inaweza kuwa na madhara kwenye ukuaji wa uchumi
Ripoti hiyo inabainisha kuwa wastani wa bei ya bidhaa kati ya mwaka 2013 na 2017 zilikuwa chini ya kiwango cha miaka ya 2008 hadi 2012 ambapo hali hiyo imesababisha kudorora kwa uchumi katika mataifa 64 yaliyo tegemezi kwenye bidhaa huku zingine zikikwama kusonga mbele. Picha|UNCTA.
- Tanzania inategemea zaidi kusafirisha madini na vito vya thamani ili kujipatia mapato.
- Nchi hizo ni zile ambazo asilimia 60 ya thamani ya mauzo yake ya nje yanatokana na bidhaa.
- Lakini kupanda na kushuka kwa bidhaa ghafi kunazorotesha uchumi wa nchi hizo.
Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa (UN) imeitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa mataifa 102 duniani ambayo yanategemea bidhaa na mazao ghafi kwa ajili ya kukuza uchumi wake, jambo linaloziongezea changamoto ya kukabiliana na athari za kupanda na kushuka kwa bidhaa hizo.
Ripoti hiyo iliyopewa jina la Hali ya Utegemezi wa Bidhaa ya mwaka 2019 imetolewa na kamati ya maendeleo ya biashara ya Umoja wa Mataifa (UNCTAD) imeeleza kuwa mataifa hayo ni yale ambayo asilimia 60 ya thamani ya mauzo yake ya nje inatokana na bidhaa.
Katika ripoti hiyo ambayo ni ya nne tangu kuanza kutolewa mwaka 2012, imesema utegemezi wa Tanzania katika bidhaa na mazao ghafi uko zaidi katika usafirishaji wa madini, chuma na vito vya thamani.
Lakini katika usafirishaji wa mazao ghafi Tanzania inasafirisha zaidi tumbaku, imeeleza ripoti hiyo huku ikibanaibisha kuwa utegemezi huo una madhara makubwa katika ukuaji wa uchumi ulio imara hasa katika nchi zinazoendelea ambazo zina rasilimali nyingi asilia.
Mataifa yanayotegemea bidhaa huathiriwa na msukosuko wa bei kupanda na kushuka katika soko la dunia.
Zinahusiana:
- Mnada wa Kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Meli mpya Ziwa Victoria kuchochea biashara Afrika Mashariki
- Wakulima wanavyopigania bei nzuri ya mahindi Afrika Mashariki.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa wastani wa bei ya bidhaa kati ya mwaka 2013 na 2017 zilikuwa chini ya kiwango cha miaka ya 2008 hadi 2012 ambapo hali hiyo imesababisha kudorora kwa uchumi katika mataifa 64 yaliyo tegemezi kwenye bidhaa huku zingine zikikwama kusonga mbele.
“Kwa kuzingatia kuwa utegemezi wa bidhaa pekee mara nyingi huwa na madhara kwenye uchumi wa taifa, ni muhimu kuchukua hatua za dharura na kupunguza utegemezi huo ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu,” amesema Katibu Mkuu wa UNCTAD, Dk Mukhisa Kituyi wakati akichambua ripoti hiyo Mei 16, 2019.
Amesema mataifa hayo 102 ni zaidi ya nusu ya mataifa yote duniani ambayo ni 189 ambapo theluthi mbili kati ya mataifa hayo tegemezi ya bidhaa ni nchi zinazoendelea na ndiyo zinaathirika zaidi kutokana na utegemezi huo.
Hata hivyo, ripoti hiyo imetoa mapendekezo kwa mataifa yanayotegemea bidhaa kuimarisha uwezo wake wa ndani wa viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa na mazao ghafi ili kutengeneza bidhaa zilizokamirika.
Hatua hiyo itasadia kutengeneza fursa ajira na kuboresha sekta ya kilimo ambayo hutegemewa na nchi nyingi zinazoendelea.
Mathalani, baadhi ya mataifa yaliyokuwa yanategema kuuza zaidi mafuta nje ya nchi zikiwemo Oman, Saudi Arabia na Trinidad naTobago, zimeongeza wigo wao wa bidhaa zinazouza nje kwa kuongeza thamani ya bidhaa kwenye uzalishaji.