CAG apewa rungu kuwachunguza vigogo saba tume ya umwagiliaji
Watendaji wanatuhumiwa kwa kuonyesha udhaifu wa kiutendaji ndani ya tume hiyo ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za miradi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, upendeleo na kukosa umakini katika shughuli zao.
- Waziri Mkuu amesema uchunguzi wa CAG utabainisha ukweli juu ya ubadhirifu unaoikabili tume hiyo.
- Amesema miradi mingi ya tume ya umwagiliaji imejikita zaidi katika warsha na semina badala ya kuendeleza skimu za umwagiliaji.
- Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa amesema miradi mingi ya umwagiliaji ilifeli kwa sababu ya ilijengwa chini ya kiwango hususani mabwawa.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufanya uchunguzi wa kina wa ubadhirifu wa fedha za umma unaodaiwa kufanywa na Wakurugenzi saba wa Tume ya Umwagiliaji waliosimamishwa kazi kupisha uchunguzi huo.
Majaliwa pia ameagiza watumishi wengine 21 wa tume hiyo wachukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na utendaji usioridhisha kwenye miradi mbalimbali inayosimamiwa na taasisi hiyo.
Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo leo ( Mei 14, 2019) wakati wa kikao na viongozi wa tume hiyo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Mawaziri, Manaibu Waziri na Makatibu Wakuu wa wizara kadhaa ambapo amemtaka CAG afanye uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa tuhuma zinazowakabili vigogo hao.
“CAG afanye haraka uchunguzi wa kina, tunataka kujua ni nani alikuwa mlango wa ubadhirifu huu. Hatutamuonea mtu, wote watakaothibitika kuhusika na matumizi mabaya ya fedha watachukuliwa hatua,” amesema Majaliwa katika taarifa kwa wanahabari iliyotumwa na ofisi yake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo watendaji hao wameonyesha udhaifu wa kiutendaji ndani ya tume hiyo ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za miradi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, upendeleo na kukosa umakini katika shughuli zao.
Soma zaidi:
- Bunge lamtenga rasmi CAG Assad
- CAG hajaiacha salama sekta ya utalii, aibua utofauti wa takwimu za watalii
- CAG: HESLB imeshindwa kuwapata wadaiwa wa Sh1.46 trilioni
Tume hiyo imeshindwa kusimamia miradi takribani 10 katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha sekta ya umwagiliaji kushindwa kupata mafanikio yaliyotarajiwa kutokana na ubadhirifu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa umwagiliaji wa Luiche uliopo mkoa wa Kigoma unaokadiriwa kumwagilia hekta 3,000 ambao upo katika hatua za awali za utekelezaji lakini tayari pamekuwepo na matumizi mabaya ya fedha za mradi.
Inadaiwa kuwa Mkurugenzi Mkuu alitoa kibali na kulipa fedha taslimu masurufu ya jumla ya Sh100.7 milioni kwa wahandisi wa makao makuu, maafisa wa idara ya mipango, tathmini na ufuatiliaji kwenda kufanya ukaguzi badala ya kujenga. Mkaguzi wa nje alihoji uhalali wa malipo hayo na hajapata majibu hadi leo.
Majaliwa ameeleza kuwa hali ya kilimo cha umwagiliaji nchini hairidhishi na Serikali haijafurahishwa na utendaji wa tume hiyo licha ya kuwekeza nguvu kubwa hivyo anataka kuona mabadiliko.
“Miradi mingi inayotekelezwa na Tume ya Umwagiliaji nayo ina hali mbaya zaidi. Miradi mingi ya tume hiyo imejikita katika mafunzo, semina na warsha badala ya kujenga na kuendeleza skimu za umwagiliaji,” amesema Majaliwa.
Baadhi ya Watendaji wa Tume ya Umwagiliaji wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 14, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akamilishe mchakato wa kuwapata wajumbe wa bodi wa tume hiyo ambayo imemaliza muda wake.
Pia amemtaka Waziri huyo ahakikishe wizara yake inaisimamia tume kukamilisha ujenzi wa skimu zote za umwagiliaji zilizoanza kujengwa miaka ya nyuma zikiwemo za wakulima wadogo.
Lakini Hasunga ametakiwa afanye mabadiliko ya muundo wa tume hiyo na kuwa na maafisa wa umwagiliaji katika ngazi za mikoa na wilaya ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Awali, Hasunga amesema skimu zinazofanya kazi hazizidi 10 kati ya 2,678 hali iliyosababishwa na kuwepo kwa dosari katika usimamizi na pia matumizi mabaya ya fedha za miradi katika Tume ya Umwagiliaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa amesema miradi mingi ya umwagiliaji ilifeli kwa sababu ya ilijengwa chini ya kiwango hususani mabwawa na pia haikuwa ikilingana na kiasi cha fedha kilichokuwa kinatolewa.
“Mradi wa kutumia Sh2 bilioni wao wanatumia Sh4 bilioni,” amesema Prof Mbalawa.
Tanzania ina hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambacho kinaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa cha uzalishaji chakula na mazao ya biashara nchini.
Hadi Machi mwaka jana, kulikuwa na hekta 475,052 zilizokuwa zinamwagiliwa ambazo ni sawa na asilimia 1.6 tu ya eneo linalofaa kwa umwagiliaji jambo linaloacha fursa lukuki za maendeleo ya kilimo.
Nyongeza na Daniel Mwingira.