October 6, 2024

Mambo matano kuifanya Kagera kuwa kitovu cha biashara ya mipakani

Mambo hayo ni pamoja na ujenzi wa vituo vya pamoja mipakani, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mafunzo ya urasimishaji biashara ya mipakani.

  • Mambo hayo ni pamoja na ujenzi wa vituo vya pamoja mipakani, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mafunzo ya urasimishaji biashara ya mipakani. 
  • Mikakati hiyo imeanza kuwasaidia wananchi kupata tija ya mazao na bidhaa za viwandani. 
  • Mkoa wa Kagera umepakana na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda. 

Dar es Salaam. Wananchi wa mkoa wa Kagera huenda wakafaidika na fursa za biashara ya mipakani, baada ya Serikali  kusema inatekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo vya pamoja vya mipakani ili kufaidika na jiografia ya mkoa huo. 

Mkoa wa Kagera uliopo magharibi mwa Ziwa Victoria umekuwa kiungo muhimu katika nchi za Uganda, Rwanda na Burundi. 

Naibu Waiziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji amesema ili kuuwezesha mkoa huo kunufaika na fursa za kijiografia, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR), kipande cha Isaka hadi Rusumo chenye urefu wa kilomita 371 na kisha kuingia nchini Rwanda.

Reli hiyo ambayo itaanzia jijini Dar es Salaam itasaidia katika usafirishaji wa mizigo kati ya nchi hizo mbili ambapo Kagera itakuwa kiungo muhimu cha mpakani.

Mikakati mingine ni ukarabati wa barabara Lusahunga hadi Rusumo yenye urefu wa kilomita 91; mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu ambapo inatarajia kuzalisha umeme wa megawati 80 katika mto Rusumo na mradi wa vituo vya pamoja katika mipaka ya Rusumo na Mtukula kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kibiashara na nchi jirani za Rwanda na Uganda. 

Ujenzi wa reli utarahisisha usafirishaji wa mizigo hadi katika nchi za jirani za Uganda, Rwanda na Burundi. Picha|Mtandao.

Dk Kijaji ameainisha mikakati hiyo bungeni leo (Mei 14, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Halima Bulembo aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani mahususi wa kuifanya Kagera ifaidike na uchumi wa kijiografia.

Bulembo amesema mkoa wa Kagera ni mkoa pekee unaopakana na nchi nyingi za Afrika Mashariki, hivyo unaweza kuwa kituo cha biashara cha ukanda huo.  


Soma zaidi: 


Sambamba na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, Dk Kijaji amesema Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imetoa mafunzo kuhamasisha uanzishwaji wa vikundi vya kurasimisha biashara mipakani katika vituo vitatu vilivyoko katika mkoa wa Kagera 

“Vituo hivyo ni pamoja na Kabanga, Rusumo na Mtukula vinavyopakana na Uganda, Rwanda na Burundi kwa mtiririko huo. Pamoja na mambo mengine mafunzo haya yalilenga kuwajangea wananchi uwezo wa kutumia fursa za kiuchumi zilizoko kwenye mipaka ya nchi jirani,” amesema Dk Kijaji. 

Lakini mazao ya wakulima wa mkoa huo ikiwemo kahawa na baadhi ya bidhaa za viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi vinafaidika na jiografia ya mkoa wa Kagera.

Baadhi ya viwanda vinavyofaidika na jiografia ya mkoa ni pamoja na Kagera Fish Company Limited na Supreme Fish Limited vinavyosindika minofu ya samaki inayosafirishwa nje ya mipaka ya Tanzania.