October 6, 2024

NIT yapewa nguvu kusomesha marubani 10 wa ndege kwa mwaka

Lengo ni kuongeza idadi ya marubani wazawa ambao watapikwa katika Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Kwa sasa ili rubani aweze kuingia katika soko la ajira atatakiwa kusoma na kupata leseni ya biashara kwa gharama ya Sh136.6 milioni. Picha|Mtandao.


  • Lengo ni kuongeza idadi ya marubani wazawa ambao watapikwa katika Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
  • Itasaidia kuwa na uwiano mzuri wa marubani wazawa na wageni nchini. 
  • NIT imepewa ngu ya kusomesha marubani 10 kila mwaka. 

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema katika kuhakikisha kunakuwa na uwiano mzuri wa marubani wa ndege kati ya wazawa na wageni, Serikali imekipa nguvu Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kusomesha marubani 10 kila mwaka.

Kwa sasa uwiano wa marubani wazawa na wageni ni 49 kwa 51 ikiwa ni maana kuwa wazawa ni asilimia 49 ya marubani wote wanaohudumu nchini.

Mhandisi Kamwelwe ametoa maelezo hayo bungeni leo (Mei 13, 2019) wakati akifanya majumuisho ya hoja za wabunge kuhusu bajeti ya wizara yake katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 ya takriban Sh5 milioni. 

Amesema Serikali ina mikakati ya kuongeza marubani wazawa kwa kuwasomesha hapa nchini katika chuo cha NIT kupitia mradi wa Ujuzi wa Afrika Mashariki (East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP)) ambapo utatekelezwa kwa mkopo wa Dola za Marekeni 21.5 milioni (Sh49.44 bilioni) kutoka Benki ya Dunia. 

Mradi huo utaanza kutekelezwa Juni 2019, kwa mujibu wa Kamwelwe makubaliano ya fedha (Financial agreement) yamefanyika tayari. 

“Kupitia mradi huu, chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kusomesha marubani 10 kwa mwaka. Wizara yangu inafanya mawasiliano na Wizara Elimu, Sayansi na Teknolojia ili bodi ya mikopo ya elimu ya juu (HESLB)  iweze kuwakopesha wanafunzi wa kozi ya urubani,” amesema Mhandisi Kamwelwe.


Soma zaidi:


Kwa sasa ili rubani aweze kuingia katika soko la ajira atatakiwa kusoma na kupata leseni ya biashara kwa gharama ya Sh136.6 milioni. 

Serikali  ina mfuko wa kusomesha marubani ambao unasimamiwa na Mamlaka ya Usafiri  wa Anga (TCAA) ambao una uwezo wa kusomesha marubani watano hadi 10 kwa mwaka kulingana makusanyo katika mwaka husika.

Kwa mujibu wa Kamwelwe, mfuko huu mpaka sasa umesomesha marubani watano ambao wameshahitimu na wanafunzi 10 wataanza masomo oktoba 2019.