October 6, 2024

Watalii 330 kutoka China wawasili nchini kwa ziara ya siku nne

Watalii hao walipokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

  • Watalii hao walipokelewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
  • Watalii hao ni kundi la kwanza miongoni mwa watalii 10,000 wanaotarajiwa kuingia nchini mwaka huu. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewapokea watalii 330 wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji kutoka jimbo la Zhejiang, China ambao wako nchini kwa siku nne kwa ajili ya shughuli za utalii na biashara. 

Watalii hao waliowasili jana usiku katika  uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro    (KIA) ni kundi la kwanza miongoni mwa watalii 10,000 wanaotarajiwa kutembelea Tanzania mwaka huu chini ya mpango unaosimamiwa baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na kampuni ya TouchRoad International Holding Group ya China.

Akizungumza na watalii hao wakati wa chakula cha jioni jana (Mei 12, 2019) katika hoteli ya Mount Meru mkoani Arusha, Majaliwa amemshukuru Mwenyekiti wa TouchRoad International Holding Group, Liehui He kwa kuwaunganisha Watanzania na Wachina kupitia mpango wake wa kukuza utalii nchini.

“Mbali na kutuunganisha Watanzania na Wachina, tunakushukuru pia kwa kuamua kuitangaza Tanzania kuwa nchi yenye fursa nyingi za kitalii duniani,” amesema Majaliwa.

Amewapongeza watendaji wa TTB na makampuni ya utalii kwa maandalizi na mapokezi mazuri kwa watalii hao huku akimpa sifa Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kushirikiana na TouchRoad na kuifanya Tanzania ipokee watalii wengi kutoka nchi hiyo iliyopo mashariki ya mbali. 


Zinazohusiana:


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa amevitaja vivutio ambavyo watalii hao wanaweza kuvifurahia kuwa ni hifadhi za Taifa za Ngorongoro, Serengeti, Manyara, Mlima Kilimanjaro, Mahale, Katavi na amewataka waende visiwa vya Zanzibar kuona fukwe zenye mchanga mweupe na kupata marashi ya karafuu.

Akielezea ujio wa kundi hilo la kwanza la watalii, Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Devotha Mdachi amesema watalii hao wametokea nchini Djibouti ambako walikaa kwa siku moja na hapa Tanzania watakaa kwa siku nne na kisha wataelekea Bulawayo, Zimbabwe ambako watakaa kwa siku mbili na kurejea China.

China ni miongoni mwa masoko ya kimkakati ya utalii ambapo imewekwa katika kundi moja na nchi za Israel, Oman, Russia na Australia ambazo zimekuwa na mafungamano ya muda mrefu na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Waziri  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa zawadi ya picha ya tingatinga Mwenyekiti wa Kampuni  ya Touchroad Group ya China, He Liehui kwenye chakula cha usiku kilichoandaliwa kwa ajili ya watalii tokea nchini China, Mei 12, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mapema, akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Profesa Palamagamba Kabudi amesema ujio wa watalii hao ni sehemu ya mpango mkubwa wa nchi wa kuongeza watalii kutoka China unaofahamika kama ‘Tour Africa – The New Horizon’.

“Naomba niwasihi Watanzania, hii ni fursa hatuna budi kuichangamkia ili wao wafurahie utalii nchini lakini nasi tunufaike na uwepo wao,” amesema Prof. Kabudi.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesema Serikali imeamua kuwekeza zaidi katika sekta ya utalii kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili iweze kuongeza idadi ya watalii na hatimaye kukuza uchumi.

“Tuliamua kuwekeza katika nchi tano za kipaumbele cha kwanza ambazo ni Marekani, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na Italia. Sasa hivi uelekeo wetu ni China, Israel, Oman na nchi zote za Ghuba, Australia na Urusi,” amesema.

Jimbo la Zhejiang liko kusini mashariki mwa China na ni mojawapo ya majimbo yenye wakazi wengi matajiri. Pia jimbo hilo ni maarufu kwa shughuli za kilimo na linaongoza kwa uzalishaji wa chai na mazao yatokanayo na uvuvi.

Msanii wa muziki kutoka China,  Di Na akiwa amejichanganya na wasanii wa ngoma za asili nchini, kwenye chakula cha usiku kilichoandaliwa kwa ajili ya watalii wa China, Mei 12, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.