October 6, 2024

Naibu Waziri aikingia kifua benki ya kilimo Tanzania

Amesema benki hiyo haina ubaguzi katika utoaji wa mikopo kwa wanawake bali inazingatia masharti na taratibu zilizowekwa ikiwemo kuwa na vikundi vinavyotumika kama dhamana ya mkopo.

Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba amesema pesa zilizopo TADB ni za umma na anayetaka kupata mkopo katika taasisi hiyo ni lazima afuate taratibu zilizowekwa ikiwemo kuwa na dhamana. Picha|Mtandao.


  • Amesema benki hiyo haina ubaguzi katika utoaji wa mikopo kwa wanawake bali inazingatia masharti na taratibu zilizowekwa.
  • Amewataka wanawake wanaotaka mikopo katika benki hiyo wajiunge kwenye vikundi katika maeneo yao. 
  • Serikalki inaendelea kutoa hati za kimila za ardhi kwa wanawake zinazotumika kama dhamana ya kupata mikopo katika benki.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba amewataka wanawake wanaoomba mikopo katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kufuata taratibu zilizowekwa na kuachana na madai kuwa benki hiyo inatoa mikopo kwa ubaguzi kwa kuwapendelea wanawake wenye uwezo au wake za viongozi.  

Amesema pesa zilizopo TADB ni za umma na anayetaka kupata mkopo katika taasisi hiyo ni lazima afuate taratibu zilizowekwa ikiwemo kuwa na dhamana. 

Mgumba ametoa ufanunuzi huo leo (Mei 8, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga aliyeitaka Serikali itoa kauli kuhusu madai ya kuwa benki ya TADB ina tabia ya ubaguzi ya kutoa mikopo kwa wanawake wenye uwezo au wake za vigogo (Viongozi wa Serikali). 

“Siyo kweli kwamba Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo inatoa mikopo kwa kibaguzi, hii ni benki ya maendeleo, ni benki ya kimkakati na tumeianzisha maalum kuendeleza kilimo hapa nchini.

“Kwa hiyo hizi ni pesa za umma zina taratibu zake, zina masharti. Labda hao unaowaona wanapata ni wanawake waliotimiza vigezo vinavyohitajika na benki ili waweze kupata mikopo,” amesema Mgumba.

Amesema miongoni mwa masharti hayo ni wanawake kujiunga katika vikundi katika maeneo yao ambapo hutumika kama dhamana ya kupata mikopo katika benki hiyo. 

Katika swali lake, Mlinga amesema benki hiyo imekuwa na tabia ya ubaguzi inatoa mikopo kwa wanawake wenye uwezo au wake za vigogo lakini wale wanawake wenye uwezo mgodo ambao wamejiunga kwenye vikundi wanapewa masharti magumu. 


Zinazohusiana: 


Akitoa ufafanuzi, Mgumba amebainisha kuwa tayari waliielekeza benki hiyo kuwapa kipaumbele wanawake ambapo wanatakiwa kutoa asilimia 20 ya mikopo yote kwa kundi hilo. 

“Pamoja na maelekezo ya Serikali tuliwaambia mikopo wanayotoa, asilimia 20 watoe kwa akina mama lakini benki hii imeweza kutoa zaidi ya asilimia 33 ya mikopo yote waliyotoa imeenda kwa akina mama,” amesisitiza Mgumba. 

Amesema Serikali bado inawathamini wanawake ambapo imetoa fursa ya kupata mikopo katika benki za NMB  na NBC ambazo zina dirisha maalum la kutoa mikopo kwa vikundi vinavyojishughulisha na kilimo na miradi mbalimbali. 

Pia Serikali imeendelea kutoa hati miliki za kimila za ardhi kwa ajili kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi na kuzitumia hati hizo kama dhamana kukopa katika taasisi mbalimbali za kifedha. 

Mikopo hiyo wanaitumia kama mitaji ya kununua dhana bora za kilimo na pembejeo ili kuongeza uzalishaji na kuanzisha viwanda vidogo vidogo, kuongeza tija na vipato vyao. 

Kwa mujibu wa wizara ya kilimo, wanawake wanachangia silimia 90.4 ya nguvu kazi ya wanawake inayotumika katika shughuli za kilimo na huchangia wastani wa asilimia 70 ya mahitaji ya chakula nchini.