October 6, 2024

Viwanja 10 bora zaidi vya ndege duniani 2019

Katika orodha hiyo, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Changi wa nchini Singapore ndiyo unashikilia nafasi ya kwanza duniani kwa ubora kwa mwaka 2019.

  • Katika orodha hiyo, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Changi wa nchini Singapore ndiyo unashikilia nafasi ya kwanza duniani  kwa ubora kwa mwaka 2019. 
  • Unasifika zaidi kwa huduma nzuri na bustani kubwa yenye maduka, hoteli zinazotumiwa na wasafiri kwa mapumziko. 
  • Viwanja vingine ni Tokyo Haneda cha Japan, Incheon (Korea Kusini) na Doha Hamad (Qatar).

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikikamilisha ujenzi wa jengo jipya namba tatu (Terminal III) la uwanja wa ndege wa kimataifa Julius Nyerere (JNIA) ili kuongeza ufanisi na utendaji wa uwanja huo, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Changi nchini Singapore umetajwa kwa mara ya saba mfululizo kama uwanja bora zaidi duniani mwaka 2019.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka ya utafiti ya usafiri wa anga iliyotolewa na kampuni ya Skytrax Machi, 2019, Singapore imepata ushindi huo baada ya kuwapita washindani wake wakubwa, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Toky Haneda wa nchini Japan na Incheon uliopo Seoul, Korea Kusini. 

Utafiti huo ulihusisha zaidi ya wasafiri 13 milioni duniani ambapo Changi imechukua pia ushindi wa kuwa uwanja wa ndege bora zaidi wenye huduma nzuri za mapumziko kwa wasafiri.

Washikiri wa utafiti huo walitakiwa kutoa alama kwa viwanja vya ndege duniani kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo mazingira ya ukaguzi, sehemu ya kufikia wageni, maduka, usalama na uhamiaji. 

Katika vigezo hivyo, Changi ilifanikiwa kupata alama za juu kutokana na huduma nzuri ambazo zilishuhudiwa na wasafiri waliotumia uwanja huo kwa nyakati tofauti. 

UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA CHANGI SINGAPORE

                         

Lakini uwanja wa ndege wa Changi unaungana na viwanja vingine tisa kuunda orodha ya viwanja 10 bora zaidi duniani (The World Top 10 Airports of 2019) huku kati ya viwanja hivyo, sita  vinatoka katika nchi za Asia.

Nafasi ya pili imeshikiliwa na uwanja wa ndege wa Tokyo Haneda ukifuatiwa na Incheon wa Seoul. Uwanja wa ndege wa Doha Hamad wa Qatar umeshika nafasi ya nne na  Hong Kong uliopo China (nafasi ya tano).

Viwanja vingine ni Chubu Centrair (Japan) umeshikilia nafasi ya sita, Munich namba saba (Ujerumani), London Heathrow (Uingereza) nafasi ya nane, Narita wa Japan na nafasi ya 10 ni Zurich (Switzerland).   

Utafiti huo pia ulitumia vigezo vingine kupima ubora wa viwanja vya ndege duniani. Mathalan uwanja wa ndege wa Tokyo Haneda umetajwa kama uwanja msafi zaidi duniani huku London Heathrow umetajwa kama uwanja wenye jengo bora la mapokezi. 

Uwanja wa ndege wa Guangzhou wa China umetajwa kama uwanja ulioboreshwa zaidi duniani.


Zinazohusiana:


Sifa nyingine uliyoibeba uwanja wa ndege wa Changi ni kuwa na bustani kubwa yenye huduma mbalimbali ikiwemo hoteli, migahawa, maduka zaidi ya 300 na huduma za chakula cha usiku. 

Licha ya kuwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kutokuwepo kwenye orodha ya viwanja 10 bora duniani, bado una nafasi ya kufanya vizuri ikizingatiwa kuwa Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuboresha uwanja huo. 

Kukamilika kwa jengo la Terminal III kutawezesha kuhudumia ndege 17 hadi 19 zikiwemo kubwa kwa wakati mmoja na kumudu abiria milioni 6 kwa mwaka ambapo katika eneo la nje ya uwanja kuna nafasi ya kuegesha magari 2,000 ya watu wanaotumia uwanja huo.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Tkyo Haneda uliopo Japana nao unatajwa kuwa bora zaidi duniani. Picha|Mtandao.