Mengi alivyoacha alama ya uwekezaji katika teknolojia Tanzania
Miezi mitano kabla ya kifo chake alifanikiwa kufanya uwekezaji mkubwa wa takriban Sh101 bilioni wa ujenzi wa viwanda vikiwemo vya magari na simu ambao ukiendelezwa utaleta matokeo chanya katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa Mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP amefariki dunia usiku wa kuamkia leo (Mei 2,2019) mjini Dubai, Falme za Kiarabu. Picha|Mtandao.
- Miezi mitano kabla ya kifo chake alifanikiwa kufanya uwekezaji wa takriban Sh101 bilioni mkubwa wa ujenzi wa viwanda vikiwemo vya magari.
- Miradi hiyo ikikamilika itafungua fursa za ajira kwa watanzania na kuwa ukumbusho muhimu wa kuishi kwake duniani.
Wakati watanzania wakiendelea kuomboleza kifo cha Reginald Mengi, mfanyabiashara huyo ameacha alama muhimu ya uwekezaji katika sekta ya teknolojia ambayo ikiendelezwa inaweza kuwa sehemu muhimu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa Mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP amefariki dunia usiku wa kuamkia leo (Mei 2,2019) mjini Dubai, Falme za Kiarabu.
Katika robo ya mwisho ya mwaka 2018 (Oktoba hadi Disemba), Mengi alifanya uwekezaji mkubwa katika sekta tatu za mawasiliano, usafiri na mafuta ambao alitegemea kuutekeleza kikamilifu mwaka huu lakini mauti imekatisha ndoto zake.
Kiwanda cha kutengeneza simu
Oktoba 30, 2018 Mengi ambaye anamiliki vyombo vya habari takriban 11 yakiwemo magazeti, radio na runinga alitangaza kuwekeza Sh11 bilioni katika ujenzi wa kiwanda cha kwanza nchini na Afrika Mashariki cha kutengeneza simu janja katika eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam ambazo zitakazokuwa na uwezo wa kukaa na chaji kwa muda wa wiki moja na kwa wasiokuwa na umeme wanaweza chaji kwa umemejua.
Inaelezwa kuwa tayari ufungaji mitambo kwenye kiwanda hicho kinachojulikana kama IPP TouchMate umeshaanza ambapo mbali ya simu, bidhaa nyingine zitakazotengenezwa ni pamoja na tableti, kompyuta mpakato pamoja na bidhaa za kielektroniki za majumbani na vipuri vyake.
Akizungumza na wanahabari wakati wa kutangaza uwekezaji huo, Mengi alisema kiwanda hicho kitakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi na sehemu kubwa ya watakaoajiriwa ni watu wenye ulemavu.
“Simu zitakazotengenezwa na IPP TouchMate zitakuwa na uwezo wa kukaa na chaji kwa muda wa wiki moja na lengo litakuwa ni kuendana na mazingira ya maisha halisi ya Tanzania”, alinukuliwa Mengi.
Soma zaidi:
Kiwanda cha kuunda magari
Wiki tatu baadaye, Mengi alitia saini mkataba wa makubaliano baina ya kampuni yake IPP Automobile Ltd na kampuni ya Youngsan Glonet Corporation ya Korea Kusini kwa ajili ya uanzishaji wa kiwanda cha kuunganisha magari nchini.
Wakati wa utiaji saini, Mengi alisema kuwa uwekezaji huo utagharimu dola za Marekani 10 milioni (Sh22 bilioni) ambapo Oktoba mwaka huu gari la kwanza litatolewa katika kiwanda hicho cha IPP Automobile kinachojengwa eneo la Kurasini Jijini Dar es Salaam.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha magari 1,000 aina ya Kia, Hyundai na Daewoo na kutoa ajira rasmi kwa watu 500 na zisizo rasmi zaidi ya 1,000.
Uchimbaji mafuta na gesi
Mengi hakuishia kuwekeza katika simu na magari bali Disemba 10, 2018 aliongeza ushawishi wake hadi katika kampuni ya Mafuta na Gesi ya Swala ambapo aliwekeza Dola za Marekani milioni 30 (zaidi ya Sh68 bilioni) ili kuendesha shughuli za uchimbaji mafuta kuanzia mwaka huu wa 2019.
Taarifa iliyotolewa na Swala ilieleza kuwa uwekezaji huo unafanyika kupitia kampuni ya Mengi ya Energy Tanzania Limited (ETL) ambapo uwekezaji huo utajikita katika kuendeleza miradi ya awali ya vitalu vya uchimbaji mafuta nchini.
Ikiwa makubaliano hayo yatafanikiwa, ETL itamiliki hisa za asilimia 46 za kampuni ya Swala na kuwa mwanahisa mwenye sauti katika maamuzi ya kampuni hiyo.
Swala inasubiri kibali cha Serikali ili ianze shughuli za utafiti na uchimbaji wa mafuta katika kitalu cha Kito-1 katika bahari ya Hindi mwaka 2019. Katika tathmini iliyofanyika hivi karibuni, kitalu hicho kinakadiriwa kuwa na mapipa milioni 185 ya mafuta yenye thamani ya zaidi Sh22.5 trilioni.
Ikiwa uwekezaji huo aliouacha Mengi kabla ya kifo chake, utasaidia kuipaisha Tanzania kimataifa hasa kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kutengeneza simu za aina yake zinazotumia umemejua.
Lakini utasaidia kuongeza nafasi za ajira hasa kwa vijana waliobobea katika teknolojia ya kisasa, jambo litakuwa ukumbusho muhimu wa kuishi kwake duniani.