November 24, 2024

Maswali manne yanayosubiri majibu sherehe za Mei Mosi 2019

Miongoni mwa maswali hayo ni ongezeko la kima cha chini cha mishahara na kupungua kwa kodi ya mishahara.

  • Miongoni mwa maswali hayo ni ongezeko la kima cha chini cha mishahara na kupungua kwa kodi ya mishahara.
  • Lakini upandaji wa madaraja ya wafanyakazi wa umma nayo huenda ikaangaziwa.

Dar es Salaam. Ikiwa zimebaki saa chache kabla ya kufanyika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), yapo maswali manne ambayo wafanyakazi wanategemea huenda wakapatiwa majibu katika sherehe hizo. 

Katika sherehe hizo ziazozofanyika kitaifa katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya zimeandaliwa na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) huku mgeni rasmi akiwa ni Rais John Magufuli. 

Kauli mbiu ya Mei Mosi ya mwaka huu wa 2019 ni “Tanzania ya Uchumi wa Kati Inawezekana, Wakati wa Mishahara na Masilahi Bora kwa Wafanyakazi ni sasa!”

Wakati wafanyakazi wakisubiri kwa shauku Serikali itasema nini kuhusu maslahi na mustakabali wa ajira zao, www.nukta.co.tz tunakuletea maswali manne ambayo yanaweza kuteka ajenda za  maadhimisho hayo leo na ambayo wafanyakazi wanayasubiri kwa hamu.

 

Kima cha chini cha mshahara kuongezeka?

Sheria ya Taasisi za Kazi namba 7 ya mwaka 2004 kama ilivyorekebishwa mwaka 2015 inatoa fursa ya kuundwa kwa Bodi ya kima cha chini cha mshahara katika sekta ya umma na ile ya sekta binafsi ambazo zinawajibika kupanga kima cha chini cha mshahara kulingana na uwiano kati ya gharama ya maisha na uwezo wa biashara kulipa na kudumisha. 

Mpaka sasa kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa umma ni 300,000 huku sekta binafsi ikiwa na viwango mchanganyiko kutokana na sekta na baadhi vikiwa chini zaidi ya kiwango cha Serikali, kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).  Kima hicho cha chini kwa umma kilipanda mwaka 2015/16 kutoka Sh265,000 mwaka 2014/15. 

Mwaka huu Serikali itawakumbuka wafanyakazi na kuwaongezea kima cha chini cha mshahara?

Baadhi ya wafanyakazi wakipita kwa maandamano mbele ya Rais John Magufuli katika maadhimisho ya Mei Mosi 2019 jijini Mbeya. Picha|Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali.

Serikali itapandisha madaraja wafanyakazi wa umma?

Novemba 15, 2018 aliyewahi kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Mary  Mwanjelwa alisema Serikali imewapandisha madaraja watumishi wa umma 113,520 walioajiriwa mwaka 2012 katika awamu tatu, ambapo ya kwanza walipandishwa vyeo watumishi 28,049 waliokuwa wameidhinishiwa vyeo kabla ya zoezi la uhakiki wa watumishi hewa na uhakiki wa vyeti kuanzia Juni, 2016.

Awamu ya pili ilianza mwezi Novemba, 2017 na ilihusisha watumishi 59,967 ambao taarifa zao zilikuwa kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) kabla ya zuio na awamu ya tatu ilianza mwezi Aprili, 2018 na ilihusisha Watumishi 25,504 ambao barua zao zilikuwa hazijaingizwa kwenye mfumo.

Hata hivyo, Serikali iliahidi kuwapandisha vyeo wafanyakazi wa umma mpaka pale zoezi la uhakiki watumishi wa umma litakapomilika.


Soma zaidi: Wafanyakazi wengi hawajui haki zao: Ripoti


Tayari Serikali imechukua hatua mbalimbali za uhakiki watumishi wa umma ambapo mwaka 2017 ilitoa ripoti inayoonyesha kuwapo kwa watumishi wa umma wapatao 9, 932 wenye vyeti feki ambao walikuwa wanavitumia katika ajira zao, jambo ambalo ni kosa la jinai. 

Watumishi hao waliondolewa kazini na katika mfumo wa malipo, ambapo Rais John Magufuli alisema hatua hiyo imesaidia kuokoa Sh138 bilioni zilizokuwa zikilipwa kwa watumishi wasio na sifa. 

Suala la  upandishwaji vyeo kwa watumishi wa umma linazingatia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utendaji kazi mzuri, kukidhi sifa zilizoainishwa katika miundo ya maendeleo ya utumishi, uwepo wa nafasi wazi na bajeti iliyotegwa. 

Lakini katika sherehe za leo za Mei Mosi, kutakuwa na matumaini yoyote kwa wafanyakazi kupanda madaraja ya kazi?

 

Nyongeza ya mishahara itakuwepo?

Februari 7, 2019, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akijibu swali bungeni alieleza kuwa nyongeza ya mishara kwa watumishi wa umma inasubiri kukamilika kwa tathmini ya Tume ya Mishahara na Motisha ambayo inapitia kada zote za utumishi wa umma na kazi hiyo ikakimilika basi nyongeza ya mishahara itatangazwa kwa wafanyakazi wenye sifa.

WAZIRI MKUU AKITOA UFAFANUZI WA NYONGEZA YA MISHAHARA

                             

Lakini swali linabaki kuwa wafanyakazi wa umma wategemee nyongeza hiyo kutangazwa leo? 

Kodi inayokatwa katika mishahara ya wafanyakazi itapungua?

Katika sherehe za Mei Mosi mwaka 2016, Rais Magufuli alitangaza kupunguza kiwango cha kodi katika mishahara (PAYE) kutoka asilimia 11 ya wakati huo hadi tisa kilichoanza mwaka wa fedha wa 2016/17.

Hata hivyo, kwa mujibu wa viwango vya kodi vilivyopo sasa, punguzo hilo linawabeba zaidi wafanyakazi wa kada ya chini wanaolipwa mshahara unaozidi Sh170,000 hadi Sh360,000.

Lakini kwa wafanyakazi wanaolipwa mshahara zaidi ya Sh360,000 na kuendelea wanalazimika kulipa kodi ya ziada ukiondoa kodi ya msingi ya asilimia tisa.

Kodi katika mishahara ya asilimia tisa inayotumika sasa itapungua au itaongezeka?