October 6, 2024

Bajeti ya wizara ya elimu yashuka kiduchu

Makadirio ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yameshuka kutoka Sh1.406 trilioni katika mwaka 2018/2019 hadi Sh1.389 mwaka wa fedha wa 2019/2020 unaoanza Julai mwaka huu.

  • Makadirio ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yameshuka kutoka Sh1.406 trilioni katika mwaka 2018/2019 hadi Sh1.389 mwaka wa fedha wa 2019/2020 unaoanza Julai mwaka huu. 

Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ameliomba Bunge liidhinishe Sh1.389 trilioni kwa ajili matumizi ya mwaka 2019/2020 ikiwa ni pungufu kidogo kwa asilimia 1.2 ikilinganishwa na makadirio ya Sh1.406 trilioni ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 unaoishia Juni mwaka huu. 

Profesa Ndalichako, aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake leo (Aprili 29, 2019) bungeni jijini Dodoma,  amesema kati ya fedha hizo zilizoombwa, Sh826.71 bilioni au asilimia 59 ya bajeti ya wizara hiyo zitaelekezwa katika miradi ya maendeleo na fedha zilizobaki zitatumika kwa matumizi ya kawaida. 

Hata hivyo, kiasi cha fedha kilichoelekezwa katika miradi ya maendeleo kimepungua kidogo ukilinganishwa na makadirio ya mwaka huu unaoishia Juni ambapo wizara ilitenga Sh929.9 bilioni. 

Akizungumzia vipaumbele vya wizara yake katika kipindi hicho cha mwaka wa fedha ambao unaanza Julai 1 mwaka huu, Prof Ndalichako amesema pamoja na mambo mengine wanakusudia kuanzisha mfumo wa usajili shule kwa njia ya kielektroniki (Electronic accreditation system) ambao utasaidia kuboresha ufanisi wa usajili wa shule hizo. 


Zinazohusiana: 


Kipaumbele kingine katika bajeti hii kitakuwa ni kuzifanyia tathmini taasisi 5,945 zilizo chini ya wizara hiyo ambapo 4,667 ni shule za msingi, shule za sekondari (1,244) na vyuo vya ualimu 56. 

“Hatua hiyo itasaidia uboreshaji wa elimu inayotolewa katika taasisi hizo,” amesema Prof Ndalichako.

Katika kuongeza ubora katika ufundishaji, walimu 300 wa shule za sekondari watajengewa uwezo ili kuwanoa zaidi katika taaluma ya ushauri na nasaha. 

Akitoa maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa wizara hiyo, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Suzan Lyimo (Chadema) amesema Serikali iache kuchanganya fedha za mikopo ya elimu ya juu na fedha za miradi ya maendeleo kwa sababu zinaonekana ni nyingi lakini sehemu kubwa zinakwenda katika mikopo hiyo na miradi halisi inakosa fedha hizo. 

“Kwa mfano kwa mwaka huu tu (2018/2019) Sh427 bilioni sawa na asilimia 45.6 zimekwenda bodi ya mikopo. Tatizo linazidi kuwa kubwa kwa kuwa fedha za elimu ya juu zinazidi kuongezeka na kuacha miradi halisi ya maendeleo,” amesema Lyimo.

Amesema ili kuondoa mkanganyiko uliopo Serikali inashauriwa kutenga fungu maalum kwa bodi ya mikopo kama ilivyo kwa Tume ya UNESCO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu ,Sayansi na Utamaduni) ambayo ina Sh2 bilioni lakini ina fungu lake.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Juma Nkamia  ameishauri Serikali kutoa fedha za bajeti ya mwaka 2018/2019 kabla mwaka wa fedha haujaisha ili wizara ya elimu iweze kutimiza majukumu yake kwa wakati. 

Tazama zaidi kufahamu yaliyojiri katika uwasilishaji wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.