October 7, 2024

Serikali yaeleza msimamo biashara ya kubandika kucha bandia

Imesema haina mpango wa kufunga biashara za saluni za kubandika kucha bandia kwasababu hakuna taarifa za madhara ya matumizi ya kucha hizo.

Matumizi ya vipodozi vikiwemo vya kuongeza makalio na kujibadili rangi nyeusi kuwa nyeupe (mkorogo) yamekuwa maarufu kwa baadhi ya wanawake ambao wanapenda kuongoza urembo katika miili yao.Picha|Mtandao.


  • Imesema haina mpango wa kufunga biashara za saluni za kubandika kucha bandia kwasababu hakuna taarifa za madhara ya matumizi ya kucha hizo.
  • Imesema itaendelea kutoa elimu kuhusu madhara yatokanayo na bidhaa za chakula, dawa, vifaa tendanishi na vipodozi zikiwemo kucha bandia.

Dar es Salaam. Serikali imesema haina mpango wa kufunga biashara za saluni za kubandika kucha bandia baada ya kutokuwepo taarifa zozote za madhara ya matumizi ya kucha hizo zinazopendwa zaidi na baadhi ya wanawake nchini kwa ajili ya urembo.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi aliyekuwa akijibu swali bungeni leo (Aprili 29, 2019) kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali haijawahi kupokea taarifa za madhara ya kucha bandia.

“TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa) haijawahi kupokea taarifa za madhara yatokanayo na kucha za kubandika. 

“Kutokana na kutokuwepo takwimu hizi, Serikali haioni sababu ya kufunga saluni zote wala kuwachukulia hatua wanaotoa huduma hii,”amesema Dk Mwinyi wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Rukia Khasim Ahmed lililoulizwa kwa niaba yake na Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma.

Ahmed alitaka kufahamu iwapo Serikali ipo tayari kufungia biashara na saluni zote na kuwachukulia hatua kali wanaotoa huduma hizo baada ya kuwepo baadhi ya wanawake walioathirika kutokana na kutumia dawa za kuongeza makalio pamoja na matumizi ya kope na kucha bandia. 

Swali za Rukia Khasim Ahmed Kuna baadhi ya wanawake wameathirika sana na dawa za kuongeza makalio pamoja na matumizi ya kopa na kucha bandia, je Serikali ipo tayari kufungia saluni zote na kuwachukulia hatua kali wanaotoa huduma hii?

Ili kukabiliana na madhara ya matumizi ya bidhaa hizo, waziri huyo amesema wizara kupitia TFDA itaendelea kutoa elimu kwa wote na kuwahamasisha watendaji wa afya kutoa taarifa za ubora na madhara yatokanayo na bidhaa za chakula, dawa, vifaa tendanishi na vipodozi zikiwemo kucha bandia.

Dk Mwinyi amesema katika mwaka wa fedha wa 2017/18 Serikali ilipokea taarifa 238 za madhara yaliyohisiwa kutokana na matumizi ya dawa kutoka kwa watumiaji na watendaji wa afya lakini ilibainika baadaye kuwa zote ni salama.


Zinazohusiana: 


Matumizi ya vipodozi vikiwemo vya kuongeza makalio na kujibadili rangi nyeusi kuwa nyeupe (mkorogo) yamekuwa maarufu kwa baadhi ya wanawake ambao wanapenda kuongoza urembo katika miili yao.

Septemba 2018 uliibuka mjadala mkubwa Tanzania baada ya Spika wa Bunge Job Ndugai kupiga maarufuku wabunge wanawake na wageni wenye kope na kucha bandia kuingia bungeni kutokana na sababu za kiafya. 

Hata hivyo, majibu ya Serikali leo kuhusu kutokuwepo kwa takwimu za madhara ya kucha bandia huenda yakiibua upya mjadala wa matumizi ya vipodozi hivyo ambavyo pia vimekuwa vikitangazwa kwa kasi mtandaoni.